Monday, 7 April 2014

CHAMA CHA WAVUNAJI MAGOGO MSITU WA TAIFA WA SAOHILL CHASAMBARATIKA


Meneja wa Msitu wa Taifa wa Saohill, Salekh Beleko

Mkuu wa Wilaya ya Mufindi akisisitiza jambo katika mkutano wa UWASA

Baadhi ya wavunaji walioshiriki mkutano wao wa UWASA

Mwenyekiti wa UWASA, Christian Aia
CHAMA cha Wavunaji wenye Viwanda vya Mbao katika Msitu wa Taifa wa Saohill Mufindi (SAFIA) kiko katika hatua za kusambaratika baada ya wanachama wake wengi kujitoa na kuanzisha chama kipya.

Zaidi ya wavunaji 360 baadhi yao wakiwa ni wale waliokuwa wanachama wa SAFIA wameanzisha Umoja wa Wavunaji katika Msitu wa Saohill (UWASA) uliosajiliwa kisheria Septemba, mwaka jana.

Kuanzishwa kwa chama hicho kwa mujibu wa mmoja wa wanachama wake, Carlos Kinyoa kunatokana na migogoro mingi ya kiuongozi inayoiandama SAFIA, baadhi yake ikiwa imefikishwa mahakamani.

Mei, mwaka jana, viongozi watatu wa SAFIA akiwemo Mwenyekiti wa chama hicho, William Nyalusi (64), Katibu Mkuu Oscar Kaduma (42) na mjumbe Donald Ndalo (45) walifikishwa katika mahakama ya hakimu mkazi wa mkoa wa Iringa kwa makosa matatu yanayohusiana na kugushi nyaraka mbalimbali za fedha.

Viongozi hao walifikishwa mahakamani kwa kesi hiyo inayoendelea kuchunguzwa baada ya wanachama wa SAFIA kuuagiza uongozi wao wa muda chini ya Katibu Mkuu wake, Basil Tweve, kulifikisha Polisi shauri hilo la kughushi.

Wakati kesi hiyo ikiendelea katika mahakama hiyo, katika kikao cha UWASA kilichofanyika juzi kwenye ukumbi wa Halmshauri ya Wilaya ya Mufindi, mjini Mafinga baadhi ya wavunaji ambao hawataki haki zao zilizoko SAFIA zipotee bure waliibua madai mapya dhidi ya baadhi ya viongozi wa SAFIA.

Tuhuma hizo zinazohusu matumizi mabaya ya zaidi ya Sh Milioni 50 zinazotokana na makato ya asilimia mbili ya fedha wanazolipa wavunaji kwa kila mgao wa uvunaji wa miti wanaopata.

Mmoja wa wanachama wa SAFIA, Audax Mshumbushi alisema “haya madai ya Sh Milioni 50 ni mapya kabisa kwangu, mimi ni mwanachama wa SAFIA nakuhakikishia sifahamu kabisa kuhusu madai hayo.”

Akikanusha madai yanayomuhusisha na matumizi mabaya ya fedha hizo, Shumbushi alisema “mimi ni mwanachama tu, sijawahi kushiriki mambo yoyote yanayohusu matumizi ya pesa, kwahiyo wanaonihusisha na madai hayo ya matumizi ya fedha hizo ni waongo.”

Fedha hizo ambao hukusanywa na Shamba la Saohill, hukabidhiwa kwa uongozi wa SAFIA na kati yake asilimia 0.5 hutumiwa na chama hicho kuchangia shughuli za maendeleo ya elimu wilayani Mufindi, asilimia 0.5 nyingine hutumika kwa ajili ya uendeshaji wa SAFIA na asilimia moja huingizwa kwenye mfuko wa Saccos ya chama hicho.

Meneja wa Msitu wa Taifa wa Sao Hill, Salekh Beleko alisema baada ya kutokea kwa mgogoro huo SaoHill iliacha kukukusanya fedha hizo.

“Wamefunguliana kesi, na katika mazingira hayo Sao Hill iliacha kukusanya fedha hizo kwa niaba ya wavunaji hao; mimi ni mgeni hapa, lakini nimekuta maamuzi hayo yamekwishafanywa,” alisema.

Alisema pamoja na mgogoro wa wavunaji hao Sao Hill haioni shida kufanya kazi na vyama vyote viwili japokuwa kuna haja wakawa na chama kimoja chenye nguvu kwa kuwa malengo yanayofananafanana.

Mbali na Meneja wa Saohill, wengine waliohudhuri mkutano huo ni Mkuu wa Wilaya ya Mufindi Evarista Kalalu aliyesema anataka kuona maslai ya wavunaji wa miti wilayani humo yanalindwa.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment