Thursday, 3 April 2014

BUSTANI YA MANISPAA YA IRINGA KUWA KIVUTIO KIZURI CHA UTALII MKOANI IRINGA

Bustani ya Manispaa ya Iringa inavyoonekana kwa sasa
Vyakula na vinywaji vya aina mbalimbali vimeanza kutolewa kwenye bustani hiyo na kampuni ya IMARA FOODS iliyopewa tenda ya kuendeleza bustani hiyo


BUSTANI ya Halmashauri ya Manispaa ya Iringa itafanywa kuwa kivutio cha kwanza cha utalii katikati ya mji wa Iringa; hiyo ni kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa Theresia Mahongo.

Mpango huo ni jitihada za halmashauri hiyo kuunga mkono harakati za kitaifa za kuboresha shughuli za utalii nchini na hasa baada ya mkoa wa Iringa kutangazwa kuwa kitovu cha Utalii kusini mwa Tanzania.

Ili kufikia lengo hilo, Mahongo alisema mwaka jana halmashauri hiyo ilitangaza tenda kwa ajili ya kumpata mwekezaji atakayesaidia kuboresha mazingira ya bustani hiyo ili yavute watalii wa ndani na nje.

“Tunataka bustani ile iwe na hadhi kubwa, iwe na hadhi ya kimataifa itakayoleta sifa kwa manispaa yetu na taifa kwa ujumla kwa kukuza shughuli za utalii mkoani Iringa,” alisema.

Mahongo alisema mchujo ulifanywa kwa umakini mkubwa uliiwezesha kampuni ya IMARA FOODS kuibuka kidedea dhidi ya kampuni nyingine.

Aliipongeza kampuni hiyo kwa kuanza maboresho ya bustani hiyo kwa kupanda miti ya kivuli, maua na nyasi za kuteleza ili kuwavutia watalii wengi zaidi.

Afisa Utalii wa Shirika la Hifadhi ya Taifa (Tanapa) wa ofisi ya kanda ya Nyanda za Juu Kusini iliyopo mjini Iringa, Risala Kabongo alisema manispaa ya Iringa ni lango la watalii wanaokuja mkoani Iringa kutembelea vivutio mbalimbali ikiwa ni pamoja na hifadhi kubwa kuliko zote nchini ya Ruaha.

Alisema mbali na kuboresha mazingira yake, shughuli za kuboresha vivutio vya utalii zinatakiwa kwenda sambamba na ujenzi wa miundombinu mbalimbali kama ujenzi wa hoteli za kitalii na maeneo ya kupumzikia.

Mmoja wa wakurugenzi wa IMARA FOODS, Peter Christopher alisema kazi ya kuboresha bustani hiyo imeanza kwa kasi kubwa na watalii wa ndani na nje watagemee makubwa katika kipindi kifupi kijacho.

“Tutazingatia vipengele vyote vilivyopo katika mkataba wetu; tumedhamiria kuifanya manispaa ya Iringa iwe mfano wa shughuli za utalii kusini mwa Tanzania,” alisema.

Alisema mbali na kupanda maua ya kuvutia, nyasi na miti ya vivuli, katika bustani hiyo wataweka vivutio vingine mbalimbali vikiwemo vinywaji na vyakula vilivyozoelekea na vile vya kitamaduni.

“Tunajipanga kuanza kutengeneza vyakula vya kitamaduni kwasababu ni sehemu muhimu katika kukuza utalii; mfano wa vyakula hivyo ni kama ugali wa muhogo na nyama ya wanyama wadogo kama sungura na simbilisi,” alisema.

Alisema utalii wa vyakula vya asili umekuwa ukivutia watalii wengi katika miji mingine ya kitalii ukiwemo Arusha.

Alisema maboresho mengine katika bustani hiyo yatakuwa yakifanywa kwa kuzingatia mahitaji ya wadau na maelekezo ya manispaa hiyo.

Kuboreshwa kwa bustani hiyo kumeelezwa na wadau wa maendeleo ya manispaa ya Iringa kwamba kutaongeza idadi ya watalii wanaotembelea hifadhi ya Taifa ya Ruaha.

Hifadhi ya Ruaha kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Hifadhi za Taifa (Tanapa) ndiyo inayoongoza kusini mwa Tanzania kwa safari za utalii. Hifadhi ya kwanza ni Serengeti.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment