Monday, 31 March 2014

BEI CHEE YA BIASHARA YA NGONO CHUO CHA MAENDELEO YA JAMII IPOGOLO IRINGA YAWAPAGAISHA WANAUME


Saimon Keraryo wa Tacaids
Abous Msemo wa Tuko Wangapi? Tulizana
MAHOJIANO yasio rasmi yaliyofanywa katika vyuo mbalimbali mkoani Iringa yanaonesha baadhi ya wanafunzi wa kike wanaosoma katika Chuo cha Maendeleo ya Jamii cha Ipogolo mjini Iringa wanapendwa na wanaume wengi kwasababu wanafanya biashara ya ngono kwa bei chee.

Wakati mtandao wa ngono katika chuo hicho ukiwa katika hali hiyo, mahojiano hayo yanaonesha kwamba Chuo Kikuu cha Iringa (zamani Tumaini Iringa) kinasifika kwa kuwa na baadhi ya wanafunzi wa kike wanaofanya biashara ya ngono kwa bei kubwa.

Tofauti hiyo imeelezwa na Kampeni ya Tuko Wangapi? Tulizana kwamba inatokana na tofauti ya elimu baina ya wanafunzi wa vyuo hivyo.

Kuwepo kwa wanafunzi waliopo katika mtandao wa ngono kunavihusisha pia vyuo vingine vikuu vya Ruaha na Mkwawa na vyuo vingine mbalimbali vya elimu ya chini na ya kati vilivyopo mkoani Iringa.

Taarifa iliyotolewa  kwa wanahabari walioshiriki mkutano wa maandalizi ya kampeni hiyo itakayofanywa Mjini Iringa wiki hii, mmoja wa maafisa wa kampeni hiyo, Abou Msemo alisema asilimia 80 ya maambukizi ya VVU yanachochewa na watu walio katika mtandao wa ngono.

Mtandao huo kwa mujibu wa Msemo, unawahusisha wale walio na mpenzi zaidi ya mmoja katika mahusiano ya ngono.

Ikilenga kuihamasisha jamii ya watu wa Iringa hususani vijana kujiepusha na mtandao wa ngono, Msemo alisema April 5, mwaka huu Wizara ya Afya kwa kupitia kampeni hiyo inayoratibiwa na Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi (Tacaids) itayakutanisha makundi mbalimbali ya jamii katika uwanja wa Samora mjini Iringa.

Alisema wakiwa katika uwanja huo upimaji wa VVU kwa hiari utafanywa sambamba na elimu ya VVU na Ukimwi na namna ya kujikinga na maambukizi hayo.

Taarifa iliyotolewa kwa wanahabari hao na mwakilishi wa Tacaids, Saimon Keraryo inasema viashiria vya mwaka 2011 na 2012 vinaonesha kwamba maambukizi ya VVU kwa wanawake na wanaume wenye mahusiano ya ngono kwa wapenzi wengi ni asilimia 7.5.

Keraryo alisema kiwango hicho ni kikubwa kwa asilimia 2 zaidi ikilinganisha na kile cha maambukizi ya VVU miongoni mwa wanawake na wanaume wenye mahusiano na mpenzi mmoja ambacho ni asilimia 5.5.

Alisema kiwango cha ushamiri wa VVU kinachochewa pia na kushamiri kwa tabia ya wanaume wanaofanya ngono wao kwa wao na wanawake wanaopenda kufanya ngono katika umbile lao la nyuma.

Wakati mkoa wa Njombe ukiongoza kwa kuwa na asilimia 14.8 ya maambukizi ya ugonjwa huo, mkoa wa Iringa ni wa pili kwa kuwa na asilimia 9.1, ukifuatiwa na Mbeya yenye asilimia 9.0 na Dar es Salaam ni ya nne ikiwa ni asilimia 6.9.

Akizungumzia mikoa yenye maambukizi madogo ya VVU aliitaja kuwa ni Manyara wenye asiliamia 1.5 ya maambukizi, Arusha wenye asilimia 3.2 na Kigoma wenye asilimia 3.4.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment