Friday, 7 March 2014

WANAHABARI WADAI WAMECHOSHWA KUDANDIA MAGARI YA WANASIASA


Jaji Francis Mutungi
WANAHABARI wanaoripoti habari za siasa wamepaza sauti wakisema wamechoshwa kudandia magari ya wagombea na vyama vya siasa wakati wa chaguzi mbalimbali zinazofanyika nchini.

Hata hivyo wameonya kwamba hali hiyo itaendelea kama mazingira yao ya kazi yatabaki kama yalivyo hivisasa kwa wanahabari kuvaa kofia za vyama fulani vya siasa ili wapate fursa ya kuripoti habari nzuri tu za vyama hivyo.

Hali hiyo kwa mujibu wa wanahabari hao walioshiriki mkutano na msajili wa vyama vya siasa kuhusu ushiriki wa ofisi ya msajili huyo katika uchaguzi mdogo wa ubunge jimbo la Kalenga, itawanyima wananchi haki yao ya msingi ya kujua mambo mazuri na mabaya yanayotokea kwenye shughuli za wanasiasa.

"Kuna mambo mengi yanatokea katika mikutano hiyo lakini tunashindwa kutenda haki kwa kuripoti kile kinachopaswa kuripotiwa kwasababu ya mazingira magumu ya kazi hii," alisema Mpiga Mpicha Mkuu wa Gazeti la Mwananchi, Edwin Mjahuzi.

Mjahuzi aliomba ofisi ya msajili wa vyama vya siasa kwa kushirikiana na wadau wengine ikiwemo Tume ya Taifa ya Uchaguzi na walimiki wa vyombo vya habari kuangalia uwezekano wa kutoa usafiri kwa wanahabari wanaowatuma kuripoti siasa.

Naye Godfrey Mushi wa Nipashe aliitaka ofisi ya msajili wa vyama vya siasa kwa kushirikiana na tume ya taifa ya uchaguzi kuwa na kawaida ya kutoa mafunzo yanayohusu kanuni, taratibu na sheria mbalimbali zinazohusu chaguzi kabla ya kuanza kwa zoezi hilo.

Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi alisema "nimepokea maombi yenu na niwaahidi kwamba nitayafanyia kazi; tunataka kuboresha shughuli za ofisi ya msajili ili tupunguze changamoto zilizopo katika vyama vya siasa na watu wanaofanya nao kazi."

Alisema wakati ofisi yake ikijipanga kuzifanyia kazi changamoto wanazokumbana nazo wanahabari wakati wakitimiza wajibu wao kwenye shughuli za kisiasa, watafanya kongamano kubwa la wanahabari ili kwa pamoja waweze kunyumbulisha changamoto zinazowakabili na namna zinavyoweza kushughulikiwa.

Alisema uwepo wa ofisi ya msajili wa vyama vya siasa katika chaguzi mbalimbali unasaidia uchaguzi kufanyika vizuri, kwa amani na utulivu.

"Mwishowe wananchi watachagua viongozi wanaowataka; kwahiyo tunawajibu wa kuweka uwanja sawa wa ushindani katika chaguzi," alisema.

Alisema wanahabari wanatakiwa kufanya kazi kwa uhuru na akashangazwa na hatua ya baadhi yao kuripoti habari za upande mmoja..

"Nasikia kuna wanahabari wanaoripoti habari za Chadema tu, na wapo wanaoripoti habari za CCM tu; kama hali hiyo ipo inahatarisha uhuru wa vyombo vya habari na wanahabari kufanya kazi kwa misingi ya taaluma yao," alisema.

Awali Naibu Msajili, Sisty Nyahoza alisema ili uwanja wa suhindani uwe sawa ni lazima ofisi yake isaidie kuepusha matumizi makubwa ya fedha katika kampeni.

"Kuweka uwazi wa fedha na rasilimali nyingine zinazotumika katika kampeni na kuepusha matumizi ya mali za serikali katika kampeni," alisema.

Alisema katika chaguzi ndogo kama inayofanyika katika jimbo la Kalenga wagombea wanaruhusiwa kutumia kiasi kisichozidi Sh Milioni 50.

Hata hivyo akashangazwa na matumizi makubwa yanayofanywa na vyama hivyo ikiwa ni pamoja na matumizi ya helkopta na msululu wa magari tofauti na sheria inavyotaka.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment