Monday, 10 March 2014

WALIOKUWA VIONGOZI WA CHADEMA, WAKIPONDA CHAMA HICHO JIMBONI KALENGAShaibu Akwilombe na Mtera Mwampamba katika moja ya mikutano ya CCM Jimbo la Kalenga hii leo

Mwampamba akiwaponda Chadema

Mchagueni huyu, amalizie utekelezaji wa Ilani ya CCM, ndivyo alivyokuwa akisema Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, Jesca Msambatavangu

WALIOKUWA viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wamekishambulia chama hicho na viongozi wake katika mikutano ya kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge jimbo la Kalenga iliyanyika jana katika kata ya Kalenga.

Wakimnadi mgombea wa Chama cha Mapinduzi (CCM) katika mikutano mitatu tofauti iliyohudhuriwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Phillip Mangulla viongozi hao walisema viongozi wa Chadema wanatafuta ruzuku kupitia kivuli cha kuwakomboa watanzania.

Katika mikutano iliyofanyika katika vijiji vya Ipamba na Kalenga jana, aliyekuwa mjumbe wa baraza la vijana la Chadema, Mtera Mwampamba alisema wakati viongozi wa Chadema wakiudanganya umma kwamba serikali ya CCM haijafanya lolote katika utawala wake, hawaelezi fedha za ruzuku wanazopewa kwa ajili ya kuendesha chama zinatoka wapi.

"Wanapata mamilioni ya shilingi kila mwezi kutoka kwa serikali ya CCM, mamilioni hayo ndiyo yanayowafanya warushe helkopta, walipane mishahara, wanunue magari na kuendesha shughuli mbalimbali za chama zinazowanufaisha wakubwa ili wafuasi wao mikoani wakiambulia patupu," alisema.

Kama serikali ya CCM inaweza kutoa ruzuku kwa chama hicho, litakuwa jambo la ajabu wakiendelea kuwarubuni watanzania kwamba haifanyi lolote huku wao wakishindwa kuonesha mfano wa matumizi bora ya ruzuku wanayopata.

Alisema ruzuku wanayopata ni kiashiria kimojawapo kinachodhihirisha jinsi serikali ya CCM inavyotekeleza majukumu yake kwa watanzania bila kujali itikadi za kisiasa.

Aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Shaibu Akwilombe alisema Chadema inawadanya wananchi wa jimbo la Kalenga kwamba inaweza kubadili serikali na Ilani wanayotekeleza kwa kupitia uchaguzi huo mdogo.

Akwilombe ambaye kwasasa ni Katibu wa CCM wa Mkoa wa Mtwara alisema "dhana ya uchaguzi mdogo inalenga kuziba nafasi ya mtu aliyeondoka."

Alisema kabla ya uchaguzi huo, jimbo hilo lilikuwa linaongozwa na Dk William Mgimwa kupitia CCM na akawataka wana Kalenga kujaza nafasi hiyo kupitia mgombea wa chama cha CCM.

Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, Jesca Msambatavangu alisema katika mikutano hiyo kwamba "CCM hatuko tayari kuwabeba katika gari letu la maendeleo watu wa Chadema na kwamba muda wa kuachia dola haujafika."

Alisema baada ya wananchi kufanya makosa na kuwachagua wabunge 23 wa Chadema katika Uchaguzi Mkuu wa 2010 leo wameanza kujuta kutokana na mbegu ya uvunjaji wa amani inayopandikizwa.

Alisema baadhi ya vijana wameanza kuwachukia wazazi wao, vijana wenzao na serikali yao wakiamini uchochezi unaofanywa na Chadema unawaza kuleta suluhu ya matatizo yao.

"Niwaambie ukweli Chadema wakichukua jimbo hili au nchi hii, hawawezi kuwalipa mshahara kila mwezi kwasababu hamna kazi, hawawezi kuwanunulia mavazi mazuri manayovaa, hawawezi kugharamia mahitaji yenu ya kila mwezi," alisema.

Alisema vijana watapata maendeleo kwa kufanya kazi na kinachofanywa na serikali ya CCM ni kutengeneza mazingira mazuri yatakayowafanya shughuli zao ziimarike.

Alisema maendeleo hayawezi kuja kwa maandamano na akawatahadharisha vijana waanaounga mkono harakati hizo za Chadema kuwataka watoto wa wabunge na viongozi wa Chadema kushiriki maandamano yoyote yatakayoitishwa ili kama kuna kufa wafe wote.

"Pale Iringa tuna wabunge wa Chadema; kila wanapoitisha maandamano aua migomo, watoto wao hawashiriki; badala yake wanataka watoto wa masikini waingie ili madhara wapate wao," alisema.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa CCM aliwatoa hofu wana Kalenga akiwataka kujitokeza kwa wingi siku ya upigaji kura kwa kumchagua mgombea wa CCM, Godfrey Mgimwa.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment