Wednesday, 12 March 2014

WALINZI WA CHADEMA NA CCM KUDHIBITIWA UCHAGUZI MDOGO KALENGA, MAWAKALA WA PEMBEJEO WATAKIWA WARUDISHE VITAMBULISHO VYA WAPIGA KURABenson Kigaila akionesha karatasi yenye vituo vya wapiga kura vilivyoko kwenye nyumba za mabalozi wa CCM
 
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Mstaafu Damian Lubuva

Miraji Mtaturu akisisitiza jambo alipokuwa akitaka ufafanuzi wa matumizi ya helkopta ya Chadema siku ya kupiga kura
Sisi ni ndugu, siasa zisitufitinishe, hivi ndivyo anavyoonekana Kigaila akizungumza na wawakilishi wa CCM katika kikao hicho
ZIKIWA zimebaki siku tatu kufanyika kwa Uchaguzi Mdogo wa Jimbo la Kalenga wilayani Iringa Jeshi la Polisi limeahidi kuwakamata na kuwafungulia mashtaka walinzi wa vyama vya siasa watakaonekana wakizagaa karibu na vituo vya kupigia kura.

Uchaguzi huo utakaofanyika Jumapili Machi 16, mwaka huu unahusisha vyama vitatu vya siasa ambavyo ni CCM iliyomsimamisha Godfrey Mgimwa, Chadema Grace Tendega na Chausta Richard Minja.

“Kazi ya Polisi ni pamoja na kuhakikisha amani inakuwepo wakati wa zoezi la upigaji kura na utangazaji wa matokeo; sitaki kusikia habari ya vikundi vya ulinzi vya CCM Green Guard na Chadema Red Brigade,” alisema.

Aliyasema  hayo jana kwenye mkutano wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi na viongozi wa vyama vya siasa vinavyoshiriki katika uchaguzi huo, uliofanyika katika ukumbi wa Siasa ni Kilimo, mjini hapa.

Katika kikao hicho kilichoongozwa na Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Mstaafu Damian Lubuva kujadili na kushauriana kuhusu maandalizi ya mwisho ya uchaguzi huo, Mratibu wa Kampeni za CCM katika jimbo hilo, Miraji Mtaturo alitaka kupata msimamo wa tume kuhusu tangazo la Chadema linahusu matumizi ya helkopta siku ya kupiga kura.

“Mwenyekiti wenzetu Chadema wametangaza kwamba siku ya uchaguzi wataleta watu zaidi ya 1000 wakiwemo wabunge wao kwa ajili ya kulinda kura, lakini pia wamesema watatumia helkopta yao kufanya doria, hiyo haiwezi kuwa doria itakuwa ni kampeni” alisema.

Alisema matumizi ya helkopta hiyo ni kinyume na sheria ya uchaguzi inayokataza vyama kufanya kampeni siku ya uchaguzi na akata kujua kama vyama vya siasa vinaruhusiwa kuweka vikundi vyake vya ulinzi karibu na vituo vya kupigia kura.

Akijibu hoja hiyo Lubuva alisema ni muhimu kwa vyama vyote vinavyoshiriki uchaguzi huo vikazingatia sheria, kanuni na taratibu za uchaguzi.

“Machi 15 itakuwa mwisho wa kampeni za uchaguzi huo, baada ya hapo mnajua sheria inazuia vyama vya siasa na wafuasi wao kufanya kampeni siku ya kupiga kura; sitaki kuzungumzia suala la helkopta zingatieni sheria,” alisema.

Aliwataka wananchi kuondoka katika vituo vya kupigia kura mara baada ya kupiga kura kwani kazi ya kulinda na kuhesabu kura ni kazi inayofanywa na mawakala wa vyama pamoja na maafisa wa tume.

Wakati huo huo vyama vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi huo vimeainisha kero zao mbalimbali vilivyodai zinaweza kuchangia kuuharibu uchaguzi huo.

Chadema kwa kupitia mratibu wake wa kampeni wa jimbo hilo, Benson Kigaila walitaka toleo la mwaka 2010 la daftari la wapiga kura ndilo litumike katika uchaguzi huo.

“Mwenyekiti tunaambiwa kuna masahisho kadhaa yalifanywa katika daftari hilo mwaka huu 2014; masahisho hayo yalifanywa kimakosa kwasababu wadau hatukushirikishwa,” alisema.

Alisema madhara yaliyojitokeza katika masahihisho hayo yamefanya baadhi ya vituo vya kupigia kura, akatoa mfano wa kituo cha Itengulinyi  na Kaning’ombe kwamba orodha ya wapiga kura ya 2010 inatofautiana na ile 2014.

Huku akionesha nakala ya toleo la daftari hilo la mwaka 2014, Kigaila alisema kuna wapiga kura watatu wapya wameongezwa huku katika kituo cha Kaning’ombe kukiwa na ongezeko la wapiga kura wapya 24.

Akitoa ufafanuzi wa hoja hiyo, Naibu Katibu wa Tume hiyo, Dk Sisty Cariah alisema kilichofanywa na tume hiyo ni kuhakiki daftari hilo na sio kuboresha.

“Kuna baadhi ya watu waliandikishwa mwaka 2010 lakini kulikuwepo na matatizo ya hapa na pale yaliyosabisha majina yao kutoingizwa katika daftari hilo; sasa wameingizwa,” alisema.

Majibu hayo hayakukidhi kiu ya vyama vyote viwili vya siasa na ndipo Mwenyekiti wa Tume alipoamuru wawakilishi wa vyama hivyo wakutane katika kikao maalumu cha pamoja kitakachosikiliza kwa kina malalamiko ya vyama vya siasa na kuyatolea ufafanuzi.

Lingine lililoibuliwa na Chadema katika mkutano huo ni kuwepo kwa baadhi ya vituo vya kupigia kura kwenye nyumba za mabalozi wa CCM.

Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo hilo, Pedenciana Kisaka alisema dosari hiyo wameiona na wameanza kuifanyia kazi kwa kujenga vituo vya muda vya kupigia kura katika maeneo husika.

“Kazi ya kujenga vituo hivyo itafanyika kwa siku mbili, Alhamisi na Ijumaa; utaratibu wa kuwatangazia wananchi sehemu mpya watakazipigia kura umeanza,” alisema.

Hoja nyingine iliyoibuliwa na vyama vyote viwili ilihusu baadhi ya wapigakura kuwa katika hatari ya kupoteza haki yao ya msingi ya kuchagua viongozi wanaowataka kwasababu shahada zao zipo kwa mawakala wa pembejeo jimboni humo.

Mwakilishi wa CCM, Mtaturu alisema “wakati wa msimu wa kilimo wananchi wengi wamekuwa wakikopa pembejeo kwa mawakala na wamekuwa wakitumia vitambulisho vyao vya kupigia kura kuthibitisha ukazi wa maeneo yao na kujidhamini,” alisema.

Alisema baadhi ya mawakala hawataki kuwarudishia wananchi hao vitambulisho vyao hivyo kwa madai kwamba bado hawajalipwa fedha zao na hivyo kumtaka Msimamizi wa Uchaguzi kukutana haraka iwezekanavyo na mawakala hao ili wavirudishe.

Akiitikia mwito huo, msimamizi huyo alisema Ijumaa atakutana na mawakala wote wa pembejeo katika jimbo hilo lenye wapiga kura 71,765 ili kama wana vitambulisho hivyo warudishe kwa wahusika.

“Tume itafurahi kuona watu wote wenye sifa ya kupiga kura katika uchaguzi huu, wanafanya hivyo, tena bila kubugudhiwa na mtu yoyote Yule, kwahiyo tutakutana na mawakala na kuwataka wawarudishie wahusika vitambulisho vyao,” alisema.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment