Saturday, 8 March 2014

POLISI IRINGA YAKAMATA WAHAMIAJI HARAMU 46 TOKA ETHIOPIA

wahamiaji haramu 46 toka Ethiopia kama wanavyoonekana pichani baada ya kukamatwa na jeshi la Polis Iringa

Walikuwa na njaa kali, kwa msaada wa anahabari walinunuliwa mikate, soda, juice na maji

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Ramadhani Mungi akieleza jinsi wahamiaji hao walivyonaswa na kutwa nguvuni

WAHAMIAJI haramu 46 kutoka nchini Ethiopia wamekamatwa mkoani Iringa jana wakiwa wamejificha katikati ya matenga ya nyanya kwenye roli dogo la mizigo aina ya Canter.

Taarifa zilizoelezwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa,, Ramadhani Mungi kuwa ni za kiintelejensia ndizo zilizowezesha kukamatwa kwa wahamiaji hao.

"Walikuwa wakitokea mkoani Tanga wakielekea mkoani Mbeya kwa lengo la kuingia nchini Malawi wakiwa katika gari hilo lenye namba za usajili T342 AJU," alisema.

Mungi alisema ilikuwa majira ya saa 9:50 alasiri katika eneo la Gezaulole, Ruaha Mbuyuni wilayani Kilolo, wahamiaji hao walipokamatwa katika gari hilo lililokuwa likiendeshwa na Mbega Alli (37), Mbondei mkazi wa Tanga.

Alisema wahamiaji hao wanamudu kuingia nchini kwa kutumia njia za panya kwasababu mipaka ya nchi haijazungushiwa uzio tofauti na nchi zingine.

"Mifumo ya utendaji kazi ndani ya jeshi la Polisi ndiyo inayowezeshwa wahamiaji wengi kukamatwa kabla hawajatoka ndani ya nchi," alisema.

Alisema oparesheni ya jeshi hilo imewezesha mara kwa mara kukamatwa kwa wahamiaji hao wengi wao wakitokea Ethiopia na Somalia.

Alisema baada ya kumatwa wahamiaji hao wameanza kuhojiwa na kwa kushirikiana na Idara ya Uhamiaji watapelekwa mahakamani.

Wakati wahamiaji hao wakiwa hawajui lugha nyingine yoyote zaidi ya zile za kwao, mmoja wao, Shifaran aliyeonekana kumudu kuongea kingereza alisema, shughuli ya kusafirissha wahamiaji hao imekuwa ikifanywa na ndugu yake ambaye hakumtaja jina aliyeko nchini Afrika Kusini.

Alisema wahamiaji hao wamekuwa wakichukuliwa kutoka nchini kwao hadi Afrika Kusini kunakoelezwa kuwa na kazi nyingi zinazoweza kuwapatia kipato.

Alisema taarifa wanazopata, zimekuwa zikiwashawishi wengi wao kutafuta fedha na kuingia katika harakati za kukimbia nchi yao ili kubadili hali ya maisha yao.

"Hatuendi huko kwa lengo lingine zaidi ya kazi; tunalazimika kutumia mbinu mbalimbali pamoja na zile za kujifanya sisi ni wakimbizi ili tukimbie umasikini nchini kwetu," alisema.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment