Friday, 7 March 2014

MSAJILI WA VYAMA VYA SIASA AKERWA NA VIKUNDI VYA ULINZI VYA VYAMA VYA SIASA; KUSHUGHULIKIA CHANGAMOTO ZA WANAHABARI WANAPORIPOTI SIASA


Msajili wa vyama vya siasa Jaji Francis Mutungi katika kikao alichofanya na wanahabari wanaoripoti uchaguzi mdogo jimbo la Kalenga mkoani Iringa

Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza akisisitiza jambo katika kikao hicho kilichofanyika leo
Baadhi ya wanahabari walishiriki kikao hicho mbele ya meza kuu

OFISI ya Msajili wa Vyama vya Siasa Nchini imekiri kukerwa na vikundi vya ulinzi vya Chaama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Chama cha Mapinduzi (CCM).

Kwa upande wa Chadema kikundi chake kinajulikana kama Blue Guard huku cha CCM kikijulikana kwa jina la Green Guard.

Akizungumza na wanahabari hii leo kuhusu ushiriki wa ofisi hiyo katika uchaguzi mdogo wa ubunge jimbo la Kalenga, Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza alisema ofisi yake ilikwishatoa maelekezo kwa vyama hivyo kuvivunja vikundi hivyo.

"Sio kazi ya vikundi hivyo kulinda mikutano ya vyama vya siasa, kazi hiyo ni ya Polisi ambao kisheria wanaruhusiwa kutumia nguvu pale inaapowalazimu kufanya hivyo," alisema.

Alisema tofauti na Polisi vikundi hivyo haviruhusiwi kutumia nguvu na kama vitafanya hivyo vitakuwa vinavunja sheria na wahusika wake wakikamatwa wanapaswa kuchukuliwa hatua za kisheria.

"Tunakoelekea vikundi hivi vinaweza kutuletea shida katika siasa za nchi hii kwasababu vinaanzishwa kwa lengo la kutumia nguvu ili kujilinda," alisema.

Nyahoza alisema kama ilivyo kwa jesho la Polisi, ofisi yao inapenda kuona uchaguzi unakuwa huru, wa haki, amani na utulivu.

"Kwani wakati jeshi la Polisi linashughulika na watu wanaovunja sheria, ofisi ya msajili inashughulika na chama ambacho ndicho chenye jukumu la kuwaongoza wananchama na mashabiki wake," alisema.

Alisema wakati ikisimamia utekelezaji wa sheria ya vyama vya siasa, ofisi yao inasaidia kuepusha vitendo vya vurugu, matusi na uchochezi kwa kuchukua hatua stahiki kwa chama kinachohusika kwa mujibu wa sheria.

Mkutano huo ulifanyika kwa lengo la kuwaomba wanahabari wawajulishe wananchi uwepo wa ofisi hiyo katika zoezi la uchaguzi wa Kalenga, kuwafahamisha wananchi kazi zilizofanywa na ofisi hiyo tangu wafike Iringa kwa ajili ya kufuatilia uchaguzi huo.

Zingine zitakazofanywa ni kuzunguka na wagombea wote ili wapete fursa ya kuangalia mikutano ya kampeni inavyoendeshwa na namna sheria inavyozingatiwa, kufuatilia ukweli kuhusu tuhuma au malalamiko ya uvunjifu wa sheria, kutoa elimu kwa wadau wote na kusikiliza na kufanyia kazi kwa mujibu wa sheria malalamiko yatakayowasilishwa na wagombea.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment