Sunday, 30 March 2014

MILIONI 200 KUKABILIANA NA MABADILIKO YA TABIANCHI IRINGA VIJIJINI

DK Emma Liwenga

Mratibu wa Mradi, Felista Kasuga

Afisa Ardhi na Maliasili wa Halmashauari ya Wilaya ya Iringa, Donald Mshani allishukuru MMADEA kwa kuja mradi huo katika wilaya yake

Hawa ni wawakilishi walioshiriki mkutano na wataalamu kuhusu mabadiliko ya Tabianchi

ZAIDI ya Sh Milioni 200 zimetolewa kwa Shirika la Maendeleo la Mazombe Mahenge (MMADEA) la mkoani Iringa kuwawezesha wananchi wa Iringa Vijijini kukabiliana na mabadililiko ya tabianchi.

Fedha hizo zilizotolewa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mtaifa (UNDP) zitaiwezesha MMADEA inayoshirikiana na kampuni inayojishughulisha na mazingira ya E-Link kuhamasisha njia bora za kujikwamua kimaisha na usimamizi endelevu wa maliasili.

Mratibu wa Mradi, Felista Kasuga alivitaja vijiji vitakavyonufaika kuwa ni Kibebe na Weru vya kata ya Ulanda na Makatapora na Mmbweleli vya kata ya Migori.

Mwakilishi wa E-Link, Dk Emma Liwenga alisema utafiti wa awali katika vijiji vya mradi unaonesha wananchi wana uelewa kuhusiana na mabadiliko hayo pamoja na kutojua kwamba moja ya vyanzo vyake ni wao.

“Kuhusu mvua wanasema kuna tofauti kubwa ya unyeshaji hivi sasa na miaka ya nyuma; wanasema mvua zilikuwa zinaanza mwezi Oktoba mpaka April hivi sasa hazipo kwani huchelewa kuanza na kuwahi kwisha jambo linaloathiri uzalishaji katika kilimo,” alisema.

Kuhusu ongezeko la joto na ukame, alisema wananchi hao wanasema ulioanza kushamiri miaka 20 iliyopita baada ya mvua za elnino.

“Wanasema shughuli za kilimo zimetetereka na ilikuwa ni nadra kusikia kaya Fulani haina chakula, tofauti na ilivyo hivisasa ambapo pia matunda pori na wanyamapori wadogo wa asili kama digidigi na sungura wametoweka,” alisema.

Mbali na shughuli za kilimo kuathirika, wananchi wa kata ya Migori katika utafiti huo walizungumzia shughuli za uvuvi zinavyotetereka katika bwawa la Mtera ambalo kwa miaka ya karibu limekuwa linakosa maji tofauti na ilivyokuwa huko nyuma.

Alisema ukataji miti kwa matumizi ya mbao, kuni na mkaa umeharibu mazingira katika maeneo hayo na kuongeza athari za mabadiliko hayo.

Alisema mabadiliko ya tabianchi ni mabadiliko ya takwimu za hali ya hewa ya muda mrefu yanayosababishwa na ongezeko la gesijoto hasa hewa ya ukaa angani.

Alisema ongezeko hilo husababishwa na matukio ya kiasilia ya dunia na mfumo wake na shughuli mbalimbali za kibinadamu kama viwanda, kilimo, usafiri wa anga na nchi kavu.

Dk Liwenga alisema hewa hiyo inapozalishwa kwa wingi, hutengeneza utando wa hewa mfano wa blanketi ambao huruhusu tu mionzi ya jua yenye nguvu kupenya.

Akitaja malengo ya mradi, Mratibu wa Mradi, Kasuga alisema utakuza uelewa kuhusu athari za mabadiliko hayo kwa maisha ya jamii na katika maliasili na kukuza na kuhamaisisha matumizi ya elimu ya asili katika kuhifadhi mazingira na kutabiri hali ya hewa ili kukabiliana na mabadiliko hayo.

Alisema kwa kupitia mradi huo wa mwaka mmoja (Januari hadi Desemba 2014) wananchi wa vijiji hivyo wamepewa miche ya miti 20,640: miche hiyo ni ya matunda, miti ya asili na ya mbao ambayo pia ni rafiki kwa vyanzo vya maji.

Pamoja na kugawa mbolea, vifaa vya umwagiliaji na dawa za kupulizia wadudu na za kuzuia ukungu kwenye mimea kama njia ya kuwahamaisha wananchi kujikwamua kiuchumi, Kasuga alisema wamegwa mbegu za kunde, alizeti na matikiti maji katika vijiji hivyo.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment