Sunday, 9 March 2014

MGIMWA KUMBANA WAZIRI MKUU, JERRY SLAA AWA KIVUTIO KATIKA KEMPENI ZA CCM

Jerry Slaa katika jukwaa la Godfrey Mgimwa, uchaguzi mdogo jimbo la Kalenga

Mzee Nyenza akimvika mgolole wa heshima ya uchifu, Godfrey Mgimwa
WIKI ya lala salama ya kampeni za uchaguzi mdogo jimbo la Kalenga imeanza huku mgombea wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Godfrey Mgimwa akiahidi kumbana Waziri Mkuu na mawaziri wengine ili kwa pamoja wamalizie utekelezaji wa ahadi katika jimbo hilo.

Mgimwa alitoa ahadi hiyo juzi baada ya wazee wa kimila wa kata ya Mgama alikofanya mikutano minne tofauti kumpa heshima ya uchifu kwa kumvisha mgolole akiwa ameketishwa kwenye kito maarufu cha kabila la wahehe kijulikanacho kwa jina la Kigoda.

Mbali na kupewa heshima ya uchifu, mikutano ya mgombea huyo ilinogeshwa zaidi na uwepo wa mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM na Meya wa Manispaa ya Ilala, Jerry Slaa.

Baadhi ya wananchi wa kata hiyo walionekana wakimshangaa kijana huyo huku baadhi yao wakipongeza hatua ya CCM ya kuwapa madaraka nyeti vijana wadogo kama Slaa.

Mmoja wa wananchi wa kata hiyo, Nicholaus Mtafya alisema “kumbe inawezekana ndani ya CCM vijana kama hawa wakachaguliwa kushika nafasi nyeti; kama kwa Slaa imewezekana hakuna shaka kwa Godfrey Mgimwa itawezekana pia.”

Katika mikutano hiyo Slaa aliwauliza wananchi kama wanajua kwambaa serikali iliyoko madarakani ni ya CCM, aliyekuwa mbunge wa jimbo la Kalenda Dk William Mgimwa ni wa CCM na madiwani wa kata zote katika jimbo hilo ni wa CCM.

Huku wakipaza sauti katika mikutano hiyo iliyofanyika katika vijiji vya Ihemi, Ibumila na Mgama wananchi walijibu “ndio tunajua yote hayo ni ya CCM.”

Slaa alisema aliendelea kuwauliza “kama inawezekanaje katika mazingira hayo mchezaji wa yanga akaumia na kutoka nje ya  uwanja halafu timu hiyo ikaingiza mchezaji wa timu pinzani.”

Wananchi wakajibu kwamba hilo haliwezekani na katika ufafanuzi wao uliotokana na muongozo wa maswali kutoka kwa Slaa walisema akiumia mchezaji wa Yanga, mchezaji mbadala anayetakiwa kuingizwa uwanjani ni lazima awe wa Yanga.

Baada ya maelezo na maswali kwa wananchi wa vijiji vya kata hiyo, Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Iringa, Jesca Msambatavangu alisimama, kamtambulisha Godfrey Mgimwa na baadaye kumuombea kura katika staili iliyoongeza shamrashamra za mikutano hiyo.

 “Najua kila mwananchi wa jimbo hili anajua serikali iliyopo madarakani ni ya CCM na ndiyo inayotekeleza Ilani ya CCM; kwa kupitia Ilani hiyo ni lazima nipiganie utekelezaji wa ahadi zote zilizoainishwa kwa ajili ya jimbo letu,” Mgimwa alisema katika mikutano hiyo.

Alizitaja changamoto zinazoikabili kata hiyo kuwa ni pamoja na upatikanaji wa maji safi na salama, pembejeo za kilimo, miundombinu ya barabara, huduma za afya na tatizo la madawati na walimu katika shule mbalimbali.

“Baada ya uchaguzi huu kazi yangu itakuwa kumbana Waziri Mkuu na mawaziri wanaohusika na sekta zenye changamoto katika jimbo langu ili zitekelezwe kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2015,” alisema.

Aliwataka wananchi wa Jimbo la Kalenga kutoka tama baada ya aliyekuwa mbunge wao kufariki dunia kwani ana uhakika kazi iliyoanza kutekelezwa na mbunge huyo anao uwezo wa kuimalizia.

“Ninazungumza mambo ambayo nina hakika nayo; sijasimama mbele yenu kama fashion, niko mbele yenu kwasababu najua Ilani ya CCM iliahidi nini katika jimbo hili, marehemu Dk William Mgimwa aliahidi nini na mimi naahidi nini,” alisema.

Kabla ya kuvishwa mgolole kijijini Mgama, Mwenyekiti wa kijiji hicho, Mathew Mheluka alisema kabla ya kifo chake Dk Mgimwa aliahidi kuvichangia vikundi vitanoa vya sanaa Sh Milioni moja kila kimoja ahadi waliyotaka itekelezwe na Godfrey Mgimwa.

“Wana Mgama tunaahidi kukupa kura nyingi huwenda ikawa kuliko sehemu nyingine yoyote katika jimbo hili, lakini tunataka baada ya uchaguzi uangalie namna ya kutekeleza ahadi ya kutoa fedha hizo kwa vikundi vyetu,” alisema huku Mgimwa akitikisa kichwa kuashiria kukubaliana na ombi hilo.

Jukumu linguine alilopewa na wananchi wa kata hiyo ni kusaidia ujenzi wa bweni la wasichana katika shule ya sekondari Mgama.

“Marehemu Dk Mgimwa aliahidi kutusaidia; na wananchi kwa kuchangia nguvu yao tayari wamefyatua matofali, wamesogeza mchanga na mawe na kilichobaki ni kuanza kwa ujenzi wake,” alisema 

Reactions:

0 comments:

Post a Comment