Wednesday, 5 March 2014

MCHUNGAJI WA MIAKA 87 MBARONI KWA MAUAJI, WAUMINI NA WANANCHI WAITAKA POLISI IMFUTIE MASHTAKA HAYO YA UONGOMchungaji Petro Chambachamba (kushoto)
MCHUNGAJI mstaafu wa Kanisa la Anglikana Usharika wa Mfarasi kata ya Madilu wilayani Ludewa, mkoani Njombe Petro Chambachamba (87) amekamatwa na Polisi akihusishwa katika kesi ya mauaji.

Waumini wa usharika huo wamesema vyanzo vya Polisi vinavyomuhusisha mzee huyo katika kesi hiyo ni vya uongo huku wakiomba aachiwe huru kabla hawajachukua hatua nyingine.

Kwa lengo la kuongeza shinikizo hilo, wananchi zaidi ya 600 wa kijiji hicho juzi walishiriki mkutano maalumu wa kijiji kulaani hatua iliyochukuliwa na jeshi la Polisi dhidi ya mchungaji huyo na watuhumiwa wengine.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Njombe, Fulgance Ngonyani alisema pamoja na Chambachamba, watu wengine nane wamekamatwa wakihusishwa katika tukio hilo lililotokea Februari 25, mwaka huu majira saa nane mchana katika kijiji cha Mfarasi.

Alisema watu hao wanatuhumiwa kuchukua sheria mkononi kwa kumpiga hadi kumsababishia kifo Boniface Mtweve (35) mkazi wa kijiji cha Ilininda kilichopo pia katika kata ya Madilu kwa tuhuma za kuiba simu tatu mali Nuru Ngairo.

Alisema kwa kupitia taarifa za siri kutoka kwa wakazi wa kijiji hicho, Februari 28, watuhumiwa hao walikamatwa na kufikishwa mikononi mwa dola.

Wengine waliokamatwa ni Linus Chaula, Stanley Katembo, Ery Mwapinga, Kedimoni Mwapinga, Phillimon Mgimba, Richard Mvalla, Meshack Mgaya na Nuru Ngairo.

“Ushahidi wa awali unawahusisha watu hao tisa akiwemo mchungaji huyo, hata hivyo wanaweza kuachiwa huru endapo baadaye wataoonekana kutohusika na tuhuma hiyo; uchunguzi unaendelea” alisema.

Katika mkutano wa kijiji uliofanyika juzi kijijini Mfarasi, Mwenyekiti wa kijiji hicho, Petro Mwapinga alisema “ inasikitisha Polisi walivamia kijijini hapa usiku wa manane na kuwakamata ndugu zetu bila kushirikisha uongozi wa kijiji.”

Afisa Mtendaji wa Kijiji hicho, Samwel Mtewele alisema wote wanaotuhumiwa kuhusikakatika mauaji hayo ni wale waliotoa taarifa katika kituo cha Polisi cha Lugarawa wilayani Ludewa kwamba nyumba zao zilivunjwa na mali zao mbalimbali ziliibwa.

Msaidizi wa Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikani Dayosisi ya Kusini Magharibi, Michael Lugome alishangazwa na hatua ya jeshi la Polisi kumkamata mchungaji huyo na wenzake hao baada ya taarifa za nyumba zao kuvunjwa na baadhi ya mali zao kuibiwa kupelekwa Polisi.

“Taarifa tuliyopewa na kijiji inaonesha kwamba kabla ya tukio hilo la mauaji, mchungaji wetu mstaafu na watuhumiwa wengine walivunjiwa nyumba zao na kuibiwa; taarifa hizo zilipelekwa Polisi, Polisi walipaswa kuzifanyia kazi taarifa za wizi huo” alisema.

Alisema taarifa inaonesha baada ya kifo cha mtuhumiwa huyo wa ujambazi kijijini hapo, Polisi waliamua kuwakamata wahanga wa wizi kijijini hapo wakiwahusisha na mauaji hayo.

“Hili ni tukio la aina yake na yawezekana likawa la kwanza; lakini tuna swali moja tu la kujiuliza ni wapi na katika mazingira gani tukio hilo lilitokea likimuhisha mzee wa miaka 87,” alisema Mwenyekiti wa Idara ya Uinjilisti ya Dayosisi hiyo, Nicholaus Mgaya.

Mke wa Mchungaji huyo, Lea Chambachamba alisema mume wake anayeandamwa na uzee alikuwa nyumbani wakati watu wenye hasira kali kijijini hapo wakimpiga marehemu.

Alisema kabla ya tukio hilo nyumba yake ilivunjwa na kuibiwa viatu vilivyokutwa na marehemu huyo na haelewi ni kwanini anahusishwa katika mauaji hayo.

“Polisi hawajatenda haki,  mume wangu ana miaka 87, mimi nina miaka 70; mzee wa umri huo anawezaje kwenda kwenye kundi lenye watu wengi na kushiriki kumshambulia mtu?” alisema.

Baadhi ya wananchi walioshiriki mkutano huo wa kijiji kulaani wenzao kukamatwa, walikiri kumpiga marehemu huyo kwa umoja wao ili kukomesha vitendi vya ualifu katika kijiji chao.

Bosco Mhagama alisema “kijiji kilikuwa kinamsaka mwizi wake kwa muda mrefu; hatimaye siku zake zikafika; alikuwa akiiba kuku, ng’ombe, fedha, nguo, viatu na mali zingine za wanakijiji wanapokuwa mashambani.”

Selemani Mwalongo alisema wananchi zaidi ya 200 ukiwaondoa watu wanaotuhumiwa na mauaji hayo walipatwa na hasira na kumpa kipigo marehemu huyo baada ya kukamatwa.

“Alipokuwa kipigwa nia haikuwa kumuua, wananchi walitaka ataje ziliko mali anazoiba na watu anaoshirikiana nao,” alisema.

Katika maazimio yao wananchi walioshiriki mkutano huo walitaka Polisi kuwaachia watuhumiwa hao kwa kile walichodai sio wahusika wa tukio hilo.

Wananchi hao walisikika wakisema kama wanataka kuwakamata wahusika wa tukio hilo wakamate kijiji kizima kwasababu walioshiriki kumpiga jambazi huyo walikuwa zaidi ya 200.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment