Monday, 31 March 2014

KISWAGA ATUNISHA MTAJI WA SILC YA TANANGOZI

Kiswaga akimkabidhi Madati mchango huo

Baadhi ya wanachama wa muungano huo

Akitoa nasaha kabla ya kutoa mchango huo
MDAU wa maendeleo ya wananchi wa mkoa wa Iringa, Jackson Kiswaga ametoa mchango wa Sh 500,000 kwa muungano wa vikundi vya kuweka na kukopa (SILC) wa kijiji cha Tanangozi, Iringa Vijijini.

Kiswaga ambaye pia ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Simu za Mkononi ya Tigo wa Nyanda za Juu Kusini alitoa mchango huo juzi wakati SILC hiyo inayoundwa na vikundi 10 vyenye jumla ya wanachama 300 ikifanya mkutano wake wa kawaida kijijini hapo.

Akitoa mchango huo Kiswaga ambaye ni mwenyeji wa jimbo la Kalenga alimuomba Mungu ampe maisha marefu na amzidishie anachopata ili kiweze kuwanufaisha na wengine.

Katika shughuli zinazohusu jamii kijijini hapo, mchango huo unakuwa wa nne wa kimaendeleo kutolewa na Kiswaga.

Michango mingine aliyotoa ni pamoja na kulipa Sh Milioni 1.5 kwa ajili ya kurudisha umeme uliokuwa umekatwa katika shule ya sekondari kijijini hapo, kusomesha watoto yatima na kugharamia elimu ya ujasiriamali kwa muungano huo.

“Mimi ni mkazi wa Iringa na katika maisha yangu ya kila siku ninajiona ni sehemu ya maendeleo ya watu wa mkoa wa Iringa; nimekuwa nikisaidia na nitaendelea kufanya hivyo kwa kipindi chote nitakachokuwa hai na nitakapokuwa na nafasi ya kufanya hivyo,” alisema.

Kiswaga alisema ataendelea kutoa michango yake ya hali na mali kwa muungano huo na akaahidi kutafakari kwa kina ombi la muungano huo linalomtaka awe mlezi wake.

“Nitatafakari ombi hilo, lakini ni muhimu mkajua kwamba mimi ni mlezi wa vikundi mbalimbali mkoani Iringa, na haitoshi tu mtu akaitwa mlezi kama atakuwa hana msaada wowote wa kikundi husika,” alisema.

Akimshukuru Kiswaga kwa mchango huo, Katibu wa muungano huo, Madati Madati alisema hauna mahusiano yoyote na mambo ya kisiasa.

"Tunakaribisha wadau wote bila kujali itikadi zozote za kisiasa. Kama ilivyofanywa na Kiswaga na wengine wote wanaweza kufanya hivyo hivyo," alisema.

Alisema walipokuwa wanaanza mapema mwaka jana, walianza na mtaji wa Sh 100,000 lakini hivisasa mtaji wao umepanda hadi Sh Milioni 30.

Alisema muungano huo unatoa mikopo ya ujenzi, elimu, matibabu, biashara na dharula ambayo hurudishwa kwa riba ya asilimia 10 kwa miezi mitatu.

Alisema mipango ya baadaye ya Muungano huo ni kutoa mikopo mikubwa ya ujenzi wa nyumba bora kwa wanachama wake na akawataka wadau wengine wajitokeze kuwasaidia.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment