Tuesday, 18 March 2014

HOSPITALI YA MAFINGA LAWAMANI KWA KUCHELEWESHA HUDUMA

wateja wakisubiri huduma katika hospitali hiyo
Hospitali ya Wilaya ya Mufindi inavyoonekana pichani

UKOSEFU wa huduma mbalimbali za afya katika hospitali ya wilaya ya Mufindi iliyopo mjini Mafinga, imeelezwa kuhatarisha maisha ya wagonjwa wanaokwenda hapo kwa matibabu.

Wafikapo hospitali hapo wengi wao wanalazimika kutumia zaidi ya saa tisa kusikilizwa tu pamoja na kukosa huduma wanazohitaji.

Moja ya mambo yanayochangia ucheleweshaji na ukosefu wa huduma ni tabia inayoelezwa kukosa muarubaini inayowahusisha baadhi ya watoa huduma kufanya mambo yao badala ya kazi inayowaingizia mkono kinywani kila mwezi.

Kero hiyo inawagharimu zaidi wanawake wajawazito na wale wenye watoto wadogo wanaotakiwa kupata matibabu bure kwa kuzingatia sera ya afya ya 2007.

“Mara nyingi duka la kutolea dawa huwa halina watoa huduma na hata wakiwepo mara nyingi huwa tunakosa dawa tunazohitaji,” alisema mmoja wao aliyejitambulisha kwa jina la mama Diana.

Mganga Mkuu wa hospitali hiyo Eriki Bakuzi amekanusha madai ya wagonjwa kuchelewa kupata huduma.

Pamoja na uchache wao na tatizo la miundombinu ya hospitali hiyo,amesema watoa huduma katika hospitali hiyo wanajitahidi sana kuwahudumia wateja wao.

Wakati mganga huyo mkuu akikanusha lawama za wateja wao, Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Evarista Kalalu amekiri kupokea malalamiko ya huduma mbovu kutoka kwa wagonjwa.

Kalalu amewataka watoa huduma wasiotaka kufanya kazi na kuzingatia maadili ya kazi yao kuacha kazi kama wanashindwa kutekeleza majukumu yao.

Amesema serikali haaitasita kuwachukulia hatua za kinidhamu endapo wataendelea na tabia hiyo na akawataka wazingatie maadili wanapotoa huduma kwa wateja wao.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment