Monday, 10 March 2014

GODFREY MGIMWA AKUTANA NA MAKUNDI MAALUMU KAMPENI ZA UBUNGE KALENGA

Sista aliyemfundisha Dk William Mgimwa akimtambulisha Godfrey Mgimwa kwa watawa wengine wa misheni ya Tosamaganga

Masista walioshiriki mkutano wa Godfrey Mgimwa
 MGOMBEA ubunge kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) katika Uchaguzi Mdogo wa Jimbo la Kalenga, Godfrey Mgimwa amezidi kuchanja mbuga katika kampeni za kuwania kiti hicho kwa kukutana na makundi maalumu jimboni humo.

Makundi aliyokutana nayo ni pamoja na lile la wafanyakazi zaidi ya 500 wa mashamba makubwa ya Tumbaku  na Masista watawa zaidi ya 100 wa misheni ya Tosamanga jimboni humo.

Sista Muuguzi Paula Msambwa (73) wa misheni hiyo alisema "nina mfahamu vizuri aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo Dk William Mgimwa kwani nilikuwa mwalimu wake akiwa darasa la kwanza hadi la nne."

Akimsifu Dk Mgimwa alisema alikuwa ni mwenye akili za kupindukia akiwa hodari zaidi kwenye somo la hisabati.

Sista Msambwa alisema aliupenda uwezo aliokuwa nao Dk Mgimwa katika masomo na akamtaka akasomee upadri, ndoto ambayo hata hivyo haikuweza kutimia.

"Leo kaja mwanae, nina hakika huyu atatufaa wana Kalenga na najua kwamba ana sifa kama za baba yake katika utaalamu wa fedha," alisema.

Akiomba kura kwa kutanguliza neno la Mungu "tumsifu Yesu Kristo", Gofrey Mgimwa alisema anayafahamu vyema mahitaji ya wana Kalenga na ataanza kazi ya kuwatumikia wananchi wa jimbo hilo kwa kuanzia pale alipoishia marehemu baba yake.

Aliwaomba watawa wa misheni hiyo kumpigia kura zao zote katika uchaguzi huo ili akawe mwakilishi wao atakayehakikisha Ilani ya CCM inatekelezwa katika jimbo hilo kama ilivyoadiwa wakati wa uchaguzi mkuu wa 2010.

Akizungumza na wafanyakazi wa mashamba makubwa ya tumbaku katika viwanja vya mkulima maarufu Kyriakos Karogeries, Mgimwa alisema "tumabaku ni moja kati ya mazao ya biashara yanayolimwa jimboni humu yanayopaswa kuendelezwa."

Alisema moja ya kazi atakazofanya mara baada ya kuchaguliwa kuwa mbunge hilo ni pamoja na kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa na wananchi wa jimbo hilo zinapata masoko.

"Ninaomba kura zenu; niaminini ili niwe mtumishi wenu bora, achaneni na porojo za wanasiasa wa vyama vya siasa wanaodai wana hamu ya kwaleteeni maendeleo wakati hawawezi hata kuchangia tripu moja ya tofali kwa ajili ya ujenzi wa zahanati na shule zetu," alisema.

Kwa upande wao wafanyakazi hao wameuondoa hofu mgombea huyo kwa kumuhakikishia kura za kutosha.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment