Monday, 17 March 2014

CHADEMA YATAKIWA KUBADILI MBINU NI BAADA YA KUBWAGWA VIBAYA UCHAGUZI MDOGO WA KALENGA

Kigaila alipokuwa akiongea na wanahabari hii leo
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimetakiwa kubadili mbinu zake za kampeni kama kinataka kuleta ushindani wa kweli wa kisiasa nchini; hayo yamesemwa na wadau wa siasa mkoani Iringa.

Tambo zao, kujiamini kwao na kila aina ya ushawishi waliotumia wakati wa kampeni za uchaguzi mdogo jimbo la Kalenga haukuweza kubadili mtizamo wa wananchi dhidi ya chama hicho.

Pamoja na kuwaita wabunge karibu wote wa chama hicho kumalizia kampeni za uchaguzi jimboni humo, kulinda kura kwa kutumia chopa na walinzi wake wa kikosi cha Red Brigade, aliyekuwa mgombea wao Grace Tendega ameambulia asilimia 20 tu ya kura zote zilizopigwa.

Mgombea wa CCM Godfrey Mgimwa amezoa asilimia 80 ya kura zote; kiwango kinachoelezwa na wachambuzi wa siasa kama adhabu dhidi ya chama hicho kinachotuhumiwa na wahasimu wao kuwa kinahamasisha vurugu.

Katika kampeni zake jimboni humo CCM iliwaomba wananchi wa jimbo hilo kutoa adhabu kwa chama hicho kwa madai kwamba kinawatia wananchi hofu ya kuendelea kuishi kwa amani na utulivu.

Kila walipopita wimbo maalumu wa CCM kwa wananchi wa jimbo hilo ulikuwa na kuwafundisha Chadema namna bora ya kuendesha siasa za kistaarabu kwa kuwanyima kura.

Maneno ya CCM yalionekana kutowanyima usingizi Chadema na katika mkutano wao wa mjini Iringa uliozungumzia jinsi chama hicho kilivyojiandaa kulinda kura zake kikiamini kitashinda, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe aliwataka wananchi wanaowaunga mkono wasilale.

Ndio, waliambiwa wasilale na badala yake wawe na chupa za maji kwa ajili ya kunawa uso pale watakapopigwa mabomu kama ushindi wao utapokonywa.

Walitakiwa wakusanyike kwa msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo, wakiwa na chupa za maji mikononi mwao na wakomae kama ushindi wao ungeporwa lakini hali haikuwa hivyo.

Waliingia mitini, Mbowe na wabunge na viongozi wengine wa chama hicho hawakuonekana hiyo ni baada ya kusoma dalili za kushindwa; wameshindwa vibaya na ndio maana baadhi ya wadau wanawataka wakae chini, watafakari na labda waje na mbinu mpya za kisiasa.

Mbinu za sasa zimeshindwa na zikiendelea kutumika, huenda itakuwa ovyooo kama ilivyotabiriwa na Dk Kitila kwenye waraka wake uliomfukuzisha chama.

Godfrey Mgimwa aliyeelezwa na Chadema kuwa ni mzungu aliyeamua kuukana uraia wake wa Tanzania na kuomba ule wa Uingereza amevalishwa viatu vya marehemu baba yake Dk William Mgimwa.

Dk Mgimwa amekuwa mmbunge wa Jimbo la Kalenga baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2010 hadi Januari 1, mwaka huu alipoaga dunia.

Ndio, wananchi wa Kalenga wamefanya maamuzi, maamuzi makubwa ambayo hayakutarajiwa na wengi; walioamini Godfrey Mgimwa angeshinda, walikuwa na mashaka kama angeweza kupata ushindi mkubwa kiasi hicho kutokana na uchanga wake katika siasa za nchi hii.

Wananchi hao hawakujali, wakasema waliofiwa ni wao,wana kilasababu ya kulia msiba wao, kuumaliza na kusonga mbele; wamemchagua Godfrey Mgimwa ili avae  viatu vya marehemu baba yake kwa kura zinazoziba midomo ya wanachadema wengi.

Ameshinda kwa kupata jumla ya kura 22,962 ambazo ni sawa na asilimia 79.32 akimuacha kwamba mbali sana mshindani wake mkubwa Grace Tendega aliyepata kura 5,853 ambazo ni sawa na asilimia 20 huku mgombea Richard Minja wa Chausta akiambulia kura 150 sawa na asilimia 0.52.

Hakuna kata hata moja ambayo Chadema ilipata kura nyingi zaidi kushinda CCM; hata ile kata ya Ifunda na Nzihi zilizoonekana kuwa ngome kuu ya chama hicho wameambulia kura chache.

La kushangaza zaidi hata kata ya Magulilwa anakotoka mgombea wao, Grace Tendega chama hicho hakikuweza kupata kura.

Katika kata ya Ifunda CCM 1,627, Chadema 601, Chausta 13, kata ya Nzihi CCM 1,793, Chadema 606, Chausta 7, kata ya Magulilwa CCM 2,065 Chadema 549 na Chausta 9, kata ya Kalenga CCM 987, Chadema 200 Chausta 2, kata ya Lyamugungwe CCM 1,585 Chadema 225 Chausta 9, Kata ya Luhota CCM 1,937 Chadema 603 Chausta 26, kata ya Mseke CCM 2,013 Chadema 678 Chausta 9, Mgama CCM 1,828 Chadema 476 na Chausta 7, Maboga CCM 2,346 Chadema 186 Chausta 13, Ulanda CCM 1,752 Chadema 313 Chausta 2, Wasa CCM 2,230 Chadema 272 Chausta 2, Kiwele CCM 1,828 Chadema 476 Chausta 7 na Lumuli CCM 1,315 Chadema 335 na Chausta 3.

Mgimwa ni mbunge mteule wa jimbo hilo anayesubiri kuapishwa, hapaswi kujisahau kwa kutekeleza yale yote aliyoahidi wakati wa kampeni zake vinginevyo na kwa historia ya jimbo la Kalenga mwaka 2015 unaweza kuwa mgumu kwake. A

Akumbuke sababu zinazofanya jimbo hilo libadili mbunge kila baada ya miaka mitano; 1995 alikuwa arehemu Steven Galinoma, 2000 akachaguliwa George Mlawa 2005 akarudishwa Steven Galinoma lakini 2010 akachaguliwa marehemu Dk William Mgimwa.


Sasa wananchi wa jimbo hilo wameonesha imani kwa Godfrey Mgimwa na katika mikutano yake aliwaambia wananchi wa jibo hilo wamuonesha imani ili awaletee maendeleo kwa kuanzia pale alipoishia marehemu baba yake. Kazi ndio imeanza, kila la kheri.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment