Tuesday, 18 March 2014

CCM MKOA WA IRINGA YAMVAA OCD WA IRINGA, YAKANUSHA PIA KUHUSIKA NA WARAKA WA SH MILIONI 560

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Ramadhani Mungi akisitiza jambo katika kikao na tume ya taifa ya uchaguzi, pembeni yake ni Kamanda wa Polisi wa Wilaya ya Iringa, Sifael Pyuza
Katibu wa CCM Mkoa wa Iringa Hassan Mtenga

ZIKIWA zimepita siku mbili tu tangu Chama cha Mapinduzi (CCM) kipate ushindi wa kishindo katika uchaguzi mdogo wa ubunge jimbo la Kalenga, chama hicho kimemrushia madongo Kamanda wa Polisi wa Wilaya ya Iringa, Sifael Pyuza kikimtuhumu kuwa na ajenda ya kukidhalilisha.

Kamanda Pyuza anatuhumiwa na chama hicho kukihusisha na mchezo mchafu wa siasa kwa kuficha watu ndani ya jengo la ofisi yake kwa ajili ya uchaguzi huo.

Akizungumza na wanahabari jana, Katibu wa CCM Mkoa wa Iringa, Hassan Mtenga alisema Machi 16, mwaka huu kamanda huyo alituma makechero wa jeshi hilo katika ofisi za CCM za mkoa wa Iringa waliotumia mabavu kupekua ofisi moja baada ya nyingine.

“Ilikuwa majira ya saa sita na nusu mchana walipokuja askari hao, tukapekuliwa kila mahali tukituhumiwa kuficha watu; kitendo hicho kimekidhalilisha chama, sisi ni chama tawala hatuwezi kufanya siasa za kihuni kiasi hicho,” alisema.

Alimtaka kamanda huyo kuwaomba radhi baada ya tuhuma yake dhidi yao kubainika haina ukweli.

“Hatuwezi kukaa kimya kwasababu tunaamini alifanya hivyo kwa lengo la kukiingiza chama cha mapinduzi katika kashfa ya mchezo mchafu wa kisiasa,” alisema.

Katika uchaguzi huo, Godfrey Mgimwa alipata ushindi wa kishindo kwa kujizolea kura 22,962 dhidi ya mgombea wa Chadema, Grace Tendega aliyepata kura 5,853 huku mgombea wa Richard Minja wa Chausta ambaye hakufanya mkutano hata mmoja wa kampeni akiambulia kura 150.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Ramadhani Mungi alisema hana taarifa yoyote kuhusiana na madai ya chama hicho lakini yupo tayari kuyapokea na kuyafanyia kazi.

“Ili nitende haki kwa pande zote mbili ni lazima nipate taarifa rasmi kutoka katika chama hicho, kwahiyo wakileta nawaahidi nitaifanyia kazi,” alisema.

Wakati huo huo, Katibu wa CCM Mkoa wa Iringa amekanusha chama hicho kuhusishwa na waraka aliodai umesambazwa na Chadema ukihusu mchanganuo wa matumizi ya Sh Milioni 560 katika uchaguzi mdogo wa jimbo la Kalenga.

“Hizo ni propaganda za kisiasa, kwanza kuna kosa hawa wenzetu wamafanya, waraka huo una anwani ya Katibu wa CCM Mkoa wa Iringa lakini chini unaonekana umesainiwa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Mwigulu Nchemba, sahihi ambayo imegushiwa,” alisema.

Alisema kuna kila dalili kwamba waraka huo uliandaliwa na Chadema kwa lengo la kuwarubuni wananchi wa jimbo la Kalenga wakose imani na CCM.

Katika waraka huo wenye kichwa cha habari kinachosema ‘Malipo ya kamati mbalimbali kwenye ushindi wa jimbo la Kalenga, umeidhinisha fedha hizo zitolewe kwa viongozi mbalimbali kama walivyoomba oili zitumike katika kampeni za jimbo.

“Unataarifiwa kwamba mmetumiwa Sh 560,000,000 kwa ajili ya timu ya ushindi wiki hii ya mwisho ya kampeni, fedha hizo zimetumwa kutokana na tathimini yenu kuwa ni hali mbaya kwetu kwa barua yenu yenye  kumb Namba  CCM/IR/VOL11/096.

“Hakikisha kiwango hiki kinwafikia  walengwa wote wafuatao kwa uwiao tuliokubaliana kulingana na maeneo yao na wao wazigawe kwa mabalozi wetu kwenye kila kitongoji na kata apewe Balozi Sh850,000, Mama Galinoma Sh Milioni 80, Mama Ray (Ulanda) Sh Milioni 60, wenyeviti wa kata wa CCM kila mmoja Sh Milioni 20, makatibu wa kata kila mmoja Sh Milioni 8, makatibu wenezi CCM kila mmoja Sh Milioni 14 na Kamati ya ushindi Nzihi Sh Milioni 108,” sehemu ya waraka huo inasema.

Mtenga alisema lengo la kusambazwa kwa waraka huo lilikuwa kuwaaminisha wapiga kura wa Kalenga kwamba kuna fedha zimetolewa na CCM kwa ajili yao lakini zimeliwa na watu wanaotajwa katika waraka huo.

“Chadema wanajua CCM imeshindaje uchaguzi huu, sio kwa kugawa fedha, ni kwasababu ya mtandao wake na imani kubwa ya wananchi waliyonayo kwao,” alisema.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment