Sunday, 23 March 2014

BAJAJ ZA KIKWETE ZASHINDWA KUKABILI CHANGAMOTO YA USAFIRI KWA WAJAZITO-HII NI MOJA KATI YA MAKALA TATU ZILIZONIINGIZA KWENYE TUZO ZA UMAHIRI WA UANDISHI WA HABARI 2013

Bajaj hii ilikutwa katika Zahanati ya kijiji cha Lihonji wilayani Nachingwea mkoani Lindi ikiwa imebakia abiria badala ya wagonjwa

Mganga Mkuu wa Kituo cha Afya cha Ikizu, wilayani Bunda Mkoani Mara, Dk Abahehe Kanora akionesha bajaj iliyokataliwa na wagonjwa

Hii ni moja kati ya bajaj tatu zilizokuwa zimetolewa kwa halmashauri ya Njombe, mpaka Januari, 2013 ilikuwa haijaunganishwa ili ifanye kazi yake
Na Frank Leonard
Kazi hii ni ya mwaka 2013

WAKATI wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2010, Rais Jakaya Kikwete aliahidi kusambaza pikipiki za matairi matatu (bajaj) zipatazo 400,000 katika hospitali, zahanati na vituo vya afya nchini kwa nia ya kusaidia kusafirisha wagonjwa hususani wanawake wajawazito wanapokaribia kujifungua.

Ahadi hiyo ya Rais ilianza kutekelezwa mapema mwaka jana kwa halmashauri nyingi kupata mgao wa bajaj tatu aina ya eRanger.

Hata hivyo katika baadhi ya maeneo zilikopelekwa, ushahidi unaonesha zimeshindwa kufanya kazi iliyokusudiwa; Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Iringa Chiku Abwao (Chadema) ameahidi kuuliza swali bungeni kuhusu ufanisi wake.

“Nitajaribu kutumia fursa ya maswali ya papo kwa papo kumuuliza Waziri Mkuu kuhusu maendeleo na ufanisi wa mpango wa usambazaji na matumizi ya bajaj hizo,” Abwao anasema.

Maria Kasege (20) ni mmoja kati ya wajawazito wengi nchini wanaoshindwa kufika katika vituo vya kutolea huduma kwa wakati kutokana na tatizo la usafiri wa uhakika na miundombinu mibovu ya barabara.

Anaishi kilomita 18 kutoka hospitali teule ya Rufaa ya Ilembula; barabara ya kuelekea katika kijiji chake cha Lugoda wilayani Wanging’ombe mkoani Njombe, haipitiki kwa kuwa ina mashimo.

Alitumia saa sita kutembea kwa miguu kufika hospitalini hapo: zilikuwa zimesalia siku saba kabla hajajifungua; alijifungua Oktoba 4, mwaka jana.

Maria anasema kijiji chao hakina huduma ya usafiri wa umma na hajui kama vituo vya kutolea huduma vinatakiwa kuwa na magari ya kubeba wagonjwa; usafiri wanaoutegemea hivisasa ni wa pikipiki za kukodi ambao hata hivyo umelata nafuu kwa wenye fedha. 

“Kwa kuwa nilitembea kwa miguu kwa zaidi ya saa sita kufika hospitali ya Ilembula, nilichoka, nilipoteza nguvu na badala ya kujifungua kawaida nilifanyiwa upasuaji kwa ushauri wa daktari,” anasema.

Kama ilivyo kwa halmashauri nyingine, Afisa Mipango wa Halmashauri ya Wilaya ya Njombe, Shadrack Muhagama anasema Mei mwaka 2012, walipokea pikipiki (Bajaj) pikipiki hizo.

Oktoba mwaka jana, mbili kati ya bajaj hizo zilipelekwa katika kijiji cha Makoga (halmashauri ya wilaya ya Njombe) na Kichiwa (halmashauri ya wilaya ya Wanging’ombe).

Kijiji cha Lugoda hakikunufaika na mgao huo pamoja na kwamba hadi Januari mwaka huu, katika yadi ya halmshauri ya wilaya ya Njombe ikiwa haijaunganishwa.

Pamoja na kupelekwa katika vijiji hivyo, Muhagama anasema bajaj hizo zina tatizo la kiufundi linalopunguza ufanisi wake katika kuhudumia wagonjwa.

“Huwezi kukata kona upande wa kushoto kwasababu kitanda chake kinafika tairi la mbele, na ni shida kuzitumia kwenye barabara za vumbi, zenye kona, miinuko, na mawe,” anasema.
  
Muhagama anasema kutokana na matatizo yake hayo waliyoyaripoti pia Idara ya Usalama wa Taifa, matumizi yake yanawapa hofu wagonjwa.

Huko wilayani Bunda mkoani Mara, Mganga Mkuu wa wilaya hiyo, Dk Rainer Kapinga anasema Bajaj hizo zimepelekwa katika vituo vya afya vya Kasanda, Ikizu na Mgeta.

Hata hivyo, Mganga Mkuu wa Kituo cha Afya Ikizu, Dk Abahehe Kanora anasema bajaj waliyopokea imeshindwa kufanya kazi iliyokusudiwa.

“Wagonjwa pamoja na wajawazito wanahitaji usafiri wa uhakika wa kuwafikisha katika kituo hiki, lakini wengi waliopelekewa bajaj hii walikataa kuitumia,” anasema.

Anasema ikiwa imeunganishwa na kitanda chake Bajaj hiyo ilikuwa ikitumia zaidi ya masaa mawili katika eneo linalofikika chini ya saa moja kwa usafiri wa pikipiki ya kawaida (bodaboda) na ni shida zaidi kuitumia wakati wa mvua.

“Kwa kuwa imekataliwa, tumeamua kubadili matumizi, tumevua kitanda chake cha kulaza mgonjwa na sasa inatumika kama pikipiki ya kawaida ikisaidia shughuli za utawala; kwa taarifa kituo hiki hakina gari toka mwaka 1996,” anasema.

Anasema gari lililokuwepo (Toyota Pickup) liliuzwa mwaka 1996 baada ya kuharibika na katika kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2010, Rais Kikwete aliahidi kukipatia kituo hicho gari la wagonjwa ambalo halijatolewa mpaka sasa.

Wiki ya mwisho ya Agosti 2012 katika kijiji cha Kambumbu, wilayani Bunda, Agnes Baraka (23) anasema alitarajia kupata mtoto wake wa pili.

Kituo cha afya Ikuzu ni kituo cha jirani kilichopo Km 3 kutoka Kambumbu; barabara ya kuelekea huko nay a kuelekea hospitali ya jirani iliyopo Km 25 kutoka kijijini hapo, inapitika kwa shida kwasababu ina mashimo.

Agnes na familia yake wanasema walisikia kuhusu ujio wa bajaj ya kubeba wagonjwa katika kituo cha afya cha Ikuzu; walipiga simu lakini bajaj haikufika kumchukua.

“Nililazimika kutumia Sh 5,000 kukodi pikipiki ya kawaida (bodaboda) iliyonipeleka hadi kituo cha afya Ikizu, hata hivyo nilala siku moja na kuandikiwa rufaa kwenda hospitali teule ya wilaya ya Bunda,” anasema.

Agnes anasema alitumia Sh 50,000 kukodi gari ndogo (maarufu kwa jina la mchomoko) hadi Hospitali Teule ya Wilaya ya Bunda (DDH).

“Pamoja na kutumia gharama hiyo, mtoto alifariki baada ya kufanyiwa upasuaji, niliambiwa alikaa vibaya na nilikuwa na ugonjwa wa zinaa; sikupata matibabu ya ugonjwa huo wa Kisonono, lakini nilitoa Sh 16,000 kununua nyuzi za kushonea baada ya upasuaji” anasema.

Mwenyekiti wa kitongoji cha Kambumbu, Kiharata Warioba anasema kero ya usafiri si tu kwamba inasibu wajawazito pekee,  bali pia waume zao wanaotakiwa kuwasindikiza wake zao wakati wa kujifungua.

Warioba anasema kero hiyo inaongeza mahitaji ya wakunga wa jadi katika vijiji vyao na wakaomba serikali iwatambue na iwape vitendea kazi.

“Ni gharama kwenda kituo cha afya Ikizu au hospitali teule ya Bunda kupata huduma, pamoja na gharama ya usafiri kuwa kubwa, tunanunua vifaatiba na dawa; hii ni kero inayoweza kuondolewa na wakunga wa jadi wenye ujuzi,” anasema.

Mariam Mkumbaru na Belinda Mtandi ni wanahabari wenye taarifa zinazofanana ya jinsi bajaj hizo zisivyotumika kwa kazi zilizokusudiwa.

Septemba mwaka jana wanahabari hao walikuwa wakifanya uchunguzi wa habari za afya katika mikoa ya Lindi na Manyara kupitia program ya Fellowship inayodhaminiwa na Mfuko wa Vyombo vya Habari Tanzania (TMF).

Akiwa katika kijiji cha Lihonji wilayani Nachingwea mkoani Lindi, Mwanahabari Mariam wa gazeti la Uhuru Dar es Salaam anasema alishuhudia moja ya Bajaj iliyotolewa kwa matumizi ya kubeba wagonjwa, ikisambaza dawa ikiwa imebakia abiria wengine wawili.

Mganga wa Zahanati ya kijiji hicho, Deus Mosha alinukuliwa na mwanahabari huyo akisema kwamba Bajaj hiyo haijawahi kubeba wajawazito kwasababu inatumia muda mrefu kusafiri kwenye barabara mbovu.

“Mganga huyo anasema wajawazito hawataki kusafirishwa na Bajaj hiyo wakiwa wamelazwa katika kitanda chake kwa kuwa wanaogopa maumivu ya mgongo,” Mkumbaru anasema.

Akiwa katika kijiji cha Merelani wilayani Simanjiro mkoani Manyara, Mwanahabari Belinda wa Kili FM ya mjini Moshi anasema aliikuta Bajaj iliyotolewa na Rais kwa ajili ya kubeba wajawazito ikibeba maji kwa matumizi ya Zahanati na watumishi wake.

Kwa mujibu wa Belinda, Mganga wa Kituo cha Afya cha Mererani, Emanuel Mushi anasema baada ya kufanya kazi zingine za kiutawala, bajaj hiyo hutumika kubeba maji kwa matumizi ya kituo hicho.

Wazo la kutumia bajaj hizo kama usafiri wa kubeba wagonjwa sio geni; Uingereza, Ufaransa na Marekani walitumia wakati wa Vita ya Kwanza ya Dunia mwaka 1914 hadi 1918 kubeba wahanga wa vita hiyo.

Barani Afrika, Tanzania sio nchi ya kwanza kuanza kutumia aina hiyo ya usafiri kubeba wagonjwa; baadhi ya nchi zilizoanza ni pamoja na Malawi, Afrika Kusini, Kenya, Ethipia, Uganda na Zambia.

Hata hivyo, nchini Malawi ambako bajaj hizo zilianza mwaka 2005, zimesaidia kuongeza idadi ya wajawazito wanaojifungua katika vituo vya kutolea huduma kutoka asilimia 25 hadi 49 katika kipindi cha miaka minne.

Kwa mujibu wa Shirika la Kuhudumia Watoto Duniani (Unicef), huduma hiyo ilisaidia kupunguza vifo vya wajawazito kutoka 586 hadi 236 kwa kila wajawazito 100,000.

Katika taarifa zake za mara kwa mara, Shirika la Afya Duniani (WHO) linasema vyombo vya usafiri kama magari, pikipiki, usafiri wa majini na angani ni muhimu katika kufikia Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs) yanayoelekeza kupunguza kwa asilimia 75, vifo vya wajawazito na watoto ifikapo 2015.

Kwa mujibu wa ripoti ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ya mwaka 2009, kiasi cha wanawake wajawazito 454 katika kila 100,000 hufa hospitalini nchini Tanzania wakati wa kujifungua kutokana na matatizo yanayohusiana na usafiri, ukosefu wa elimu, vifaatiba na dawa, watoa huduma wenye ujuzi na mengineyo.

Hata hivyo taarifa ya Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal aliyotoa Januari mwaka huu wakati akifungua Mkutano wa Afya ya Mama jijini Arusha, inaonesha kwamba vifo hivyo vimepungua kwa asilimia 50 na kufikia 250.

Katika mkutano huo, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hussein Mwinyi anasema lengo ni kupunguza vifo hivyo na kufikia 193 ifikapo mwaka 2015 ambao ndio mwaka wa mwisho wa utekelezaji wa Malengo ya Millenia. 


Kwa mujibu wa WHO, usafiri ni nyenzo muhimu sana katika kuboresha na kuzifikia huduma bora za afya. Unawawezesha watu kuzifikia huduma na watoa huduma kuifikia jamii hususani ya maeneo ya mbali ya vijijini.

Usafiri ni muhimu pia kwa usambazaji wa vifaa tiba na madawa, watoa huduma katika vituo vya kutolea huduma, na kwa kusafirisha wagonjwa kati ya kituo kimoja na kingine chenye huduma bora zaidi.

WHO inasema wajawazito wakizifikia huduma za kliniki kwa wakati watakuwa wamepiga moja ya hatua muhimu zinazoweza kutoa matokeo muhimu ya kupunguzavifo vya wajawazito na watoto.

Shirika hilo limependekeza kwamba kila mjamzito hatakiwi kupata chini ya mara nne huduma za kliniki katika kipindi cha ujauzito; huduma hizo ni ushauri, kupima magonjwa mbalimbali pamoja na Virusi vya Ukimwi, matibabu na utambuzi wa hatari za kiafya kwa mjamzito.

Wanaharakati wa haki za binadamu wanasema kuna haja mambo yanayohusu ujauzito yakafikishwa kwenye vyombo vya sheria ili kuishinikiza serikali kuongeza bajeti ya afya ya uzazi itakayosaidia kupunguza vifo vya wajawazito.

Mratibu wa Kituo cha Wasaidizi wa Kisheria kwa Wanawake na Watoto Mkoani Iringa, Jackson Gaso anasema ni muhimu kukawepo na sheria itakayohusu haki ya mwanamke kabla na wakati wa kujifungua.

Kaimu Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Njombe, Dk Conrad Ugonile anasema matatizo katika sekta ya afya ni mengi, hata hivyo tatizo la wajawazito kushindwa kufika katika vituo vya kutolea huduma ni kubwa linalohitaji kupatiwa ufumbuzi utakaoleta suluhu.

Akizungumza na Mtendaji Mkuu wa shirika la kimataifa lisilokuwa la kiserikali la Pathfinder International, Dk Purnima Mane, Ikulu, Dar es Salaam Julai 19, 2012, Rais Kikwete anasema ni jambo lisilokubalika kwa mwanamke kupoteza maisha wakati akijifungua kwa sababu ujauzito siyo ugonjwa.

Miongoni mwa maamuzi ambayo Serikali imechukua kukabiliana na tatizo hilo, Rais anasema ni pamoja na kupunguza umbali wa kufikia huduma za afya kwa kujenga zahanati kila kijiji na kituo cha afya kila kata.

Serikali pia imeamua kuwa kila kituo cha kutolea huduma lazima kiwe na huduma za uzazi na wajawazito na kuzidisha harakati za kukabiliana na ugonjwa wa Ukimwi ambao ni moja ya chimbuko kubwa la vifo vya wajawazito.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment