Friday, 7 February 2014

WANA CCM TISA WAJITOKEZA KUWANIA KALENGA, YUMO PIA MTOTO WA MAREHEMU DK WILLIAM MGIMWA

Baadhi ya wagombea wa CCM Jimbo la Kalenga wakitoka ndani ya ofisi ya CCM Wilaya ya Iringa walikofanyiwa semina elekezi kabla ya kula za maoni kesho

WANACHAMA tisa wa Chama cha Mapinduzi (CCM) akiwemo mtoto wa aliyekuwa Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa, Godfrey Mgimwa wamejitokeza kuchukua fomu kuwania ubunge katika jimbo Kalenga.

Kura za maoni zitakazompata mshindi atayakepeperusha bendera ya chama hicho dhidi ya vyama vingine vya siasa, zitafanyika kesho Jumamosi.

Katibu wa CCM Wilaya ya Iringa, Amina Imbo alisema kura hizo za maoni zitafanyika katika ukumbi wa shule ya sekondari ya Mwembetogwa mjini Iringa.

Alisema tofauti na ilivyokuwa mwaka 2010 ambapo wagombea wa chama hicho walipita kila kata na kujinadi kwa wanachama wote wa CCM, utaratibu utakaotumika katika kikao hicho cha Jumamosi ni kwa wajumbe wa mkutano mkuu wa wilaya kupiga kura hizo.

Zoezi la uchukuaji na urejeshaji fomu ulifanywa kwa siku mbili Februari 5-6, mwaka huu.

“Wagombea walipewa siku mbili za kuchukua na kurejesha fomu, na kesho jumamosi, kura za maoni zitapigwa,” alisema.

Tangu Novemba 2010, jimbo hilo lilikuwa likiongozwa na Dk Mgimwa aliyefariki dunia Januari 1, mwaka huu katika hospitali ya Kloof Medic-clinic, Pretoria Afrika Kusini alikokuwa akitibiwa.

Mbali na mtoto huyo wa Dk Mgimwa, wengine waliojitokeza kupitia chama hicho ni Jackson Kiswaga, Hafsa Mtasiwa, Gabriel Kalinga, Peter Mtisi, Edward Mtakimo, Bryson Kibasa na Thomas Mwakoka.

Msimamizi wa Uchaguzi wa Wilaya ya Iringa, Pudenciana Kisaka alisema uchaguzi mdogo katika jimbo hilo utafanyika Machi 16, mwaka huu.

Kwa upande wa wagombea kutoka katika vyama vitakavyoshiriki, alisema fomu za uteuzi zitatolewa Februari 9 hadi 18.

Alisema uteuzi wa wagombea utafanyika Februari 18 na kampeni za uchaguzi huo zitaanza mara baada ya uteuzi Februari 19 hadi Machi 15.

Alisema dafatari la wapiga kura litakalotumika katika uchaguzi huo ni lile lililotumika mwaka 2010 linaloonesha jimbo hilo lina wapiga kura 85,051 na akawataka wapiga kura kujitokeza kwa wingi siku itakapofika ili waweze kupata mwakilishi wanayemtaka.

Akiwa katika ziara ya kukijenga chama mapema wiki hii, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana alitangaza sifa za mgombea ubunge atakayerithi kiti hicho kilichoachwa wazi na Dk Mgimwa.

 “Ni muhimu mbunge mtakayemchagua awe yule atakayeweza kuvaa viatu vya Dk Mgimwa, awe mtaratibu,muungwana, mnyenyekevu na mchapa kazi mwenye weledi, uzalendo na uadilifu,” alisema.

Alisema wana Kalenga wanatakiwa kuchagua mbunge msikivu kwa watu na atakaye kuwa tayari kumalizia a ahadi za maendeleo zilizoahidiwa na marehemu Dk Mgimwa.

“Nina wahakikishieni CCM ina hazina kubwa ya watu wenye sifa kama alizokuwa nazo Dk Mgimwa. Muda ukifika tutawaletea mgombea mwenye sifa kama hizo,” alisema.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment