Saturday, 1 February 2014

USHOGA NA UKAHABA WAONGEZEKA MJINI IRINGA

Mstahiki Meya wa Manispaa ya Iringa, Amani Mwamwindi
 BIASHARA ya ngono imeelezwa kushika kasi mjini Iringa huku vijana wakiume wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja nao wakiongezeka.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk Christine Ishengoma ameiagiza
Halmashauri ya manispaa ya Iringa kutumia vyombo vya dola kuwasaka watu hao na kuwafikisha kwenye mikono ya sheria.

Taarifa ya ongezeko la biashara hiyo, iliyotolewa juzi na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Iringa, Amani Mwamwindi kwenye kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Iringa (RCC) kilichofanyika katika ukumbi wa siasa ni kilimo mjini Iringa.

“Miaka ya karibuni tulikuwa tukisikia kuongezeka kwa biashara ya ushoga na ukahaba katika miji mikubwa ya Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, Morogoro na Dodoma,” alisema.

Alisema uchunguzi wao unaonesha bishara hiyo imeanza kushamiri mjini Iringa na kushauri uanzishwe mkakati wa makusudi wa kukabiliana nayo.

Mstahiki Meya alisema anao ushahidi wa kutosha uliokusanywa na idara ya halmshauri yake inayohusika na vita dhidi ya maambukizi ya virusi vya Ukimwi.

Akitoa maelekezo kwa halmshauri hiyo alisema mbali na kuwafikisha kwenye vyombo vya dola, wanaofanya  biashara hizo wanatakiwa kusaidiwa kwa kupewa elimu ili waachane na biashara hiyo.

“Elimu pekee yake inaweza isiwafae kitu, angalieni pia namna ya kuwasaidia kwa kuwatafutia miradi rafiki itakayowawezesha kujikimu katika maisha yao ya kila siku,” alisema.

Taarifa iliyotolewa mwaka jana na Mratibu wa Ukimwi wa Manispaa ya Iringa, Sikitu Mwemsi inayataja maeneo ya Mwangata na Ipogolo kuwa na idadi kubwa ya watu wanaofanya biashara hizo.

Akitoa mfano wa taarifa ya April hadi Juni 2013, Mwemsi alisema walibaini kuwepo kwa wanawake 168 wanaojiuza na wateja wao 149.

Mwemsi alisema takwimu hizo zimekuwa zikikusanywa na  halmashauri yao kupitia mradi unaojulikana kwa jina la HUSIKA.

Alisema mradi huo unalenga kuyafikia makundi yaliyopo katika hatari ya kupata maambukizi ya virusi vya Ukimwi wakiwemo mashoga.

Aliwataja watu wanaochochea biashara hiyo kuwa ni pamoja na madereva wa magari makubwa na wengine wanaonunua ngono kwa wanaojiuza.

Mkuu wa Mkoa alisema kushamiri kwa biashara hiyo kunaongeza haja kwa mkoa kuweka mkakati wa makusudi wa kupambana na dawa za kulevya, ukahaba na ushoga.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment