Sunday, 16 February 2014

TANROADS IRINGA YAKIRI KUZIDIWA NGUVU NA WAHARIBIFU WA BARABARA NDIUKA

Utengenezaji na uoshaji wa magari hayo ukiendelea kama wahusika walivyokutwa mapema hii leo
Hii ndio sehemu ya maegesho ya magari eneo la Ndiuka inavyoonekana, katikatika ni barabara kuu ya Iringa Dar 

WAKALA wa Barabara Tanzania (Tanroads) mkoa wa Iringa imekeri kuzidiwa nguvu na waharibifu wa miundombinu ya barabara eneo la Ndiuka, mjini Iringa.

Eneo la Ndiuka lipo barabara kuu ya Iringa- Dar es salaam, mita chache kabla ya kufika kituo cha Polisi cha ukaguzi wa magari Igumbilo (Igumbilo check point).

Meneja wa Tanroads mkoa wa Iringa, Mhandisi Paulo Lyakurwa ameomba msaada wa Polisi katika kukabiliana nao wahusika hao.

Aliwataja waharibifu hao kuwa ni madereva wa magari makubwa ya mizigo na vijana waosha magari hayo wanaotumia eneo la maegesho kuosha na kufanya matengenezo ya magari yao.

Alisema maafisa wa Tanroads wamekuwa wakitishiwa maisha na waharibifu hao kila wanapojaribu kuwakamata kwa kukiuka sheria za barabara.

Alisema wanaofanya matengezo, kuosha au kupata ajali huaribu  miundombinu ya barabara na kukiuka sheria ya Barabara Namba 13 ya mwaka 2007 kifungu cha 54 kinachowataka kulipa faini, kama fidia ya kukarabati au kuirejesha kama ilivyokuwa.

Alisema katika eneo la Ndiuka, barabara za maegesho ziko hatarini kuchimbika na kuharibika kutokana na kemikali za mafuta na sabuni zinazotumiwa na waharibifu hao.

Alisema wanaosha au kutengeneza magari barabarani wanatakiwa kulipa faini isiyopungua sh 500,000, huku wanaopata ajali wakilipa kulingana na tathmini ya kiwango cha uharibifu.

Alisema Tanroads imekuwa ikitumia ushahidi wa picha kuwakamata madereva wa magari makubwa katika vituo vyake vya mizani na kuwatoza faini hizo.

Lyakurwa alisema maegesho katika eneo hilo yalijengwa kuwawezesha wasafirishaji wakubwa wa mizigo kupata eneo la kumpumzika kabla ya kuendelea na safari.

“Hayakujengwa kwa ajili ya matengenezo ya magari yao wala kwa ajili ya kuosha magari yao; watambue kwamba mafuta ya magari, maji na sabuni vikikaa kwa muda mrefu barabarani vinafifisha ubora wa lami na hatimaye uharibifu,” alisema.

Alisema imekuwa vigumu kwao kukabiliana na waharibifu hao na akaomba Polisi wapunguze urasimu wanapotaka kufanya oparesheni.

“Namuomba Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa atoe idhini ya moja kwa moja pale tu tutakapohitaji askari, tupewe bila kusubiri kibali chake ili kunusuru barabara hiyo,” alisema.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk Christine Ishengoma alimuomba Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa na Mstahimi Meya wa Manispaa ya Irinnga kuwatafutia eneo mbadala vijana wanaofanya biashara ya kuosha magari katika eneo hilo.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment