Wednesday, 5 February 2014

RUSHWA YAKITHIRI IDARA ZA AFYA ZA HALMASHAURI ZA MKOA WA IRINGA

Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Iringa Emma Kuhanga akisalimia na Rais Jakaya Kikwete hivikaribuni mjini Iringa

IDARA za afya za halmashauri za wilaya za mkoa wa Iringa zimeelezwa na taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuongoza kwa kuwa na matukio mengi ya rushwa katika kipindi cha Julai 2012 hadi Juni 2013.

Wakati idara hizo ikiongoza kwa kuwa na taarifa 16 za matukio ya rushwa, ofisi ya Mkuu wa Mkoa ilifuatia kwa kuwa na taarifa saba za matukio hayo.

Mahakama inafuatia kwa kuwa na taarifa sita za matukio hayo, huku polisi na idara ya elimu zikiwa na taarifa tano, maliasili nne, mabaraza ya ardhi ya kata tatu, watendaji wa kata na vijiji moja kila moja.

Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Iringa, Emma Kuhanga alisema takwimu zinaonesha wakala wa serikali ikiwa ni pamoja na TANROADS ilikuwa na taarifa moja, TEMESA mbili wakati shirika la umma SIDO likiwa na mbili, TANESCO moja na sekta binafsi zilipatikana taarifa mbili.

Akiwasilisha taarifa hiyo kwenye kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Iringa (RCC), Kuhanga alisema jumla ya taarifa 81 zilipokelewa katika kipindi hicho

Alisema taarifa 65 kati yake zilifanyiwa uchunguzi na kufunguliwa majalada katika kipindi hicho ambacho kesi mpya zilikuwa 12 huku tano zilitolewa hukumu kwa washitakiwa kupewa adhabu ya kifungo au faini.

Alisema kazi ya kupambana na rushwa ni ngumu hasa kutokana na mtazamo hasi wa jamii  unaowaona wanaojihusisha na vitendo vya rushwa na wahujumu uchumi kuwa ni mashujaa.

Kwa upande wa mashahidi alisema, changamoto kubwa wanayopata ni kwa baadhi yao kutokuwa tayari kutoa ushahidi mahakamani kutokana na aidha kesi kuchukua muda mrefu, kutishwa au kuwa vigeugeu.

Aliitaja changamoto nyingine katika vita hiyo kuwa ni pamoja na waajiri kutosimamia maadili ya umma ya mwaka 2002 na ushirikiano hafifu na usiokuwa wa haraka toka katika baadhi ya taasisi hasa katika upatikanaji wa nyaraka muhimu na tatizo la kifedha hususani uchunguzi na uendeshaji kesi kubwa za rushwa.

Kuhanga alisema katika kupambana na changamoto hiyo wanaielimisha jamii juu ya suala zima la rushwa, Takukuru kushirikiana na vyombo vingine na kuishauri serikali kutenga fedha zaidi na kuboresha bajeti ya Takukuru ili kutokwamisha chunguzi kubwa na zenye gharama kubwa.

Wakati huo huo, Waziri wa Nchi ofisi ya Rais anayeshughulikia Utawala Bora, Kepteni Mstaafu George Mkuchika ameiagiza Takukuru kutoa mafunzo ya jinsi ya kupambana na rushwa kwa mabaraza ya madiwani nchini.

Akizungumza kwenye kikao hicho kilichofanyika kwenye ukumbi wa Siasa ni kilimo mjini Iringa, Mkuchika alisema mafunzo hayo yanatakiwa yafikishwe kwenye kata ili kuongeza chachu ya mapambano ya rushwa nchini.
Kapteni Mkuchika
 “Hayo ni maeneo ya utawala ya madiwani na ndio wanaoishi na wananchi huku miradi mingi ya maendeleo ikifanyika huko,” alisema.

Mkuchika alisema jukumu la kuzuia na kupambana na rushwa siyo la serikali peke yake bali ni la kila mwanajamii, taasisi za umma, taasisi binafsi, jumuiya za kidini pamoja na washirika wengine wa maendeleo wa kimataifa.

Alisema ni wazi kuwa rushwa ni kikwazo kikubwa cha utawala bora na dawa sahihi ya kudhibiti ni kwa kila mmoja kuzingatia maadili.


Aliongeza kuwa hatua hiyo itaiwezesha serikali kutekeleza majukumu yake ipasavyo na pia wananchi kupata huduma bora kwa wakati.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment