Tuesday, 11 February 2014

DAWA ZA KULEVYA NA ULEVI WA KUPINDUKIA VYACHOCHEA UMASIKINI IPOGOLO, IRINGA


RPC Mungi


MATUMIZI ya dawa za kulevya, pombe kupita kiasi na ngono zembe ni baadhi ya sababu zinazoelezwa na wadau wa maendeleo wa eneo la Ipogolo, mjini Iringa kusababisha umasikini miongoni mwa wakazi wa eneo hilo.

Ukosefu wa elimu umewafanya baadhi ya wakazi wa eneo hilo kujikita katika biashara hizo zinazoendelea kuathiri afya na maisha yao.

Mdau wa maendeleo ya kata hiyo aliyejitambulisha kwa jina la Samson Kibiki alisema kuna haja kwa mamlaka zinazohusika kufikisha elimu ya madhara ya mambo hayo sambamba na kumrudia na kumtumikia Mungu.

“Ni kwa kumjua Mungu, wana Ipogolo wanaweza kuepukana na matumizi ya aina hizo za biashara na matumizi yake,” alisema katika mahojiano maalumu na mtandao huu kuhusu hali za wananchi wengi wa eneo hilo.

Mmoja wa viongozi wa serikali ya eneo hilo ambaye hakutaka kutaja jina lake kwa hofu ya kubugudhiwa na vijana wanajishughulisha na bishara hiyo hadharani alisema, jeshi la Polisi linatakiwa kutuma makachero wake ili kuwanasa na kuwafikisha katika vyombo vya dola wahusika wa biashara hiyo.

Aidha alisema wanahitaji nguvu kutoka katika  uongozi wa halmashauri ya manispaa ya Iringa ili kudhibiti biashara ya uuzaji wa pombe wakati wa kazi.

“Vilabu vya pombe katika eneo hili vinafunguliwa asubuhi na vipo vinavyofanya kazi kwa masaa 24 kinyume kabisa na sheria za uendeshaji wa biashara hizo,” alisema.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Ramadhani Mungi aliipokea taarifa hiyo na kuahidi kuwasaka wafanyabishara na watumiaji wa dawa za kulevya huku akiomba ushirikiano wa wananchi.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment