Thursday, 27 February 2014

MWIGULU NCHEMBA KUZINDUA KAMPENI ZA CCM JIMBO LA KALENGA HII LEO

Mwigulu Nchemba akiteta na Godfrey Mgimwa ambaye ni mgombea ubunge jimbo la Kalenga kupitia CCM
NAIBU Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Mwigulu Nchemba leo atakuwa mgeni rasmi kwenye uzinduzi rasmi wa kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge jimbo la Kalenga.

Uchaguzi huo utafanyika Machi 6, mwaka huu baada ya aliyekuwa mbunge wake, Dk William Mgimwa kufariki dunia Januari 1, mwaka huu nchini Afrika Kusini alikokuwa akipata matibabu.

Nchemba ambaye pia ni Naibu Waziri wa Fedha ataunga na viongozi wengine wa chama hicho katika uzinduzi wa kampeni hizo utakaofanyika katika kijiji cha Ifunda, jimboni humo.

Kabla ta uzinduzi wa kampeni hizo, CCM ambayo katika uchaguzi huo imemsimamisha kada wake kijana, Godfrey Mgimwa (32) ilianza kufanya kampeni zake ilizoziita za rasharasha Febrauri 23.

Kampeni hizo za rasharasha zimekwishafanywa katika kijiji cha Mseke na kata za Kiwele (mikutano minne) na kata ya Magulilwa ambako walifanya mikutano mitatu.

Taarifa iliyotolewa na Katibu wa CCM wa Mkoa wa Iringa, Hassan Mtenga imewaomba wananchi wa kata ya Ifunda kujitokeza kwa wingi kwenye uzinduzi huo.

Wakati CCM kikizindua rasmi kampeni zake hii leo, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwa upande wake kilikwishafanya uzinduzi wake Februari 22 katika kijiji cha Kalenga.

Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Wilbroad Slaa alikuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa kampeni hizo ambazo hata hivyo zilitibuliwa na mvua kubwa iliyonyesha siku hiyo.

Baaada ya uzinduzi huo Chadema iemeendelea na mikutano yake ya kampeni katika vijiji mbalimbali vya jimbo hilo, ikimnadi mgombea wake Grace Tendega.

Chama kingine kinachoshiriki katika uchaguzi huo ni Chausta kilichomsimamisha Richard Minja; pamoja na kugombea katika jimbo hilo Minja hana ratiba yoyote ya kampeni; mpaka tunakwenda mitamboni hii leo alikuwa hajawasilisha ratiba yake ya kampeni kwa msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo, mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Iringa Pudenciana Kisika. 


Reactions:

0 comments:

Post a Comment