Wednesday, 19 February 2014

MWENYEKITI WA CCM MKOA WA IRINGA AWAJAZA MANOTI WACHEZA BAO WA STENDI YA MLANDEGE

Laki tano kweli? hatuamini macho yetu. Hivi ndivyo alivyokuwa akisema Mwenyekiti wa kikundi hicho Mendrad Nziku wakati akipokea kitita hicho toka kwa Mwenyekiti wa CCM Jesca Msambatavangu

Hapa akiteta nao na kuwahimiza umuhimu wa kuwekeza na kuweka akiba

Wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wacheza bao hao wajasiriamali
MWENYEKITI wa CCM Mkoa wa Iringa, Jesca Msambatavangu amekichangia Sh 500,000 kikundi cha wajasiriamali wa Mlandege mjini Iringa kinachoundwa na wacheza bao (draft) 154.

Mtaji wa kikundi hicho unazidi kukua siku hadi siku ikiwa ni matokeo chanya ya kuwashirikisha wadau katika shughuli zao za kila siku.

Wakati wakichangia fedha hizo, wengi wao walionekana kutoamini macho yao kwani mchango huo ulivunja rekodi ya michango yote waliyowahi kupata.

“Ndio tumekuwa tukichangiwa na wadau mbalimbali wanaokuja kututembelea, lakini wengi wao wanachanga kati ya Sh 50,000 na Sh 100,000; mchango wa mwenyekiti wa CCM ni rekodi kubwa sana katika kikundi chetu,” alisema Msemaji wa kikundi hicho, Elia Joseph.

Alisema wanachama wa kikundi hicho wanajishughulisha na shughuli mbalimbali za kiuchumi na kwamba fedha wanazochanga na kuchangiwa zitawezesha kuimarisha kikundi na wanachama wake.

Akikabidhi mchango huo, Msambatavangu alisema “ninawachangia kiasi hiki cha fedha ili ziwasaidie kupiga hatua katika shughuli zenu.”

Alisema katika kuhakikisha uchumi wa makundi ya wajasiriamali mkoani Iringa yanaimarika kiuchumi amekuwa mstari wa mbele kuwasaidia.

“Hii ni moja ya sera ya CCM ya kuwasaidia wajasiriamali kuimarisha shughuli zao; tunawafikia na tutahakikisha mnasaidiwa,” alisema.

Alisema ametoa mchango kwa kikundi hicho baada ya kuguswa na jitihada zao na akwataka wadau wengine kujitokeza na kuwasaidia.

“Tunataka kuona siku nyingine mnatuita kuja kutoa mikopo kwa wananchama wenu na hayo ndio maendeleo tunayotaka,” alisema.

Katika taarifa yao kwa Mwenyekiti huyo wa CCM, Adam Kitomo alisema kikundi kimejiwekea lengo la kujiendeleza zaidi kwa ajili ya kuanzisha chama cha kuweka na kukopa (Saccos).


“Aidha tuna mpango wa kuwa na biashara ya bodaboda na baiskeli za kukodisha; ili hayo yote yafanikiwe ni lazima nguvu ya wadau iwepo,” alisema.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment