Sunday, 2 February 2014

MWENYEKITI WA CCM MKOA WA IRINGA AWANYOSHEA KIDOLE CHA KALIPIO UVCCM

MWENYEKITI wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa, Jesca Msambatavangu amewatahadharisha vijana na kauli za kisiasa wanazotoa kwamba zinaweza kuwafanya watanzania wakachagua wagombea kutoka vyama vya upinzani.


Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, Jesca Msambatavangu (kulia)
Ametoa hadhari hiyo ikiwa ni siku chache baada ya katibu wa Uhamasishaji na Chipukizi wa Vijana wa CCM(UVCCM), Paul Makonda kumutuhumu Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kuanza mapema kampeni za kutaka kuwania urais wa 2015  hali inayokiyumbisha chama.

Ametoa onyo hilo alipokuwa akifungua Baraza Kuu la Umoja wa Vijana wa CCM Iringa Vijijini lililofanyika katika ukumbi wa siasa ni kilimo mjini Iringa.

Msambatavangu ambaye pia ni diwani wa kata ya Miyomboni mjini hapa alisema “baadhi ya vijana wana matatizo, hawajajaliwa hekima na siku zote wamekuwa wakishiriki kampeni za kuwachafua wana CCM wenzao hali inayokiweka chama katika matatizo.”

Aliwataka wana CCM kuwaepuka vijana wazushi, wenye majungu na fitina ili kuwarudisha katika mstari wa ukweli kwa kuzingatia kanuni na taratibu zinazoongoza umoja huo na chama kwa ujumla.

“Mnapowajadili wagombea kwenye vikao vyenu ni lazima mtende haki; ipo kawaida ya baadhi ya watu kutaka kuwapitisha watu wasiokubalika kwasababua ya maslai binafsi,” alisema.

Alisema kama wanaCCM watasikiliza hila za baadhi ya vijana, watakuwa wanakubali baadhi ya wanachama wenzao kutimkia vyama vya upinzani.

“Tusikubali tupungue, tusikubali wagombea wazuri ndani ya CCM wakatimkia upinzani, tukikubali tutajiweka kwenye matatizo, tuepuke hilo ili tuendelee kushika dola,” alisema.

Alisema endapo chama kitakubali kupungua kutokana na hila na kauli zinazoondoa mshikamano miongoni mwao watakuwa wanatoa fursa kwa wapinzani na ipo siku CCM inaweza kuwa chama pinzani.

“Ili tushike dola ni lazima tushinde chaguzi zote kuanzia serikali za mitaa, udiwani, ubunge na urais; na hilo litaendelea endapo wanaCCM kwa ujumla wetu tutahakikisha chama chetu kinakuwa imara na mamba yake yanajadiliwa kwa kufuata kanuni na taratibu zake,” alisema.

Alisema vijana wanatakiwa kutumia vikao kushindanisha hoja badala ya kuruhusu uzushi kumwagwa hadharani.
Akimfariji Mwenyekiti wa Chipukizi Iringa Vijijini, Menrik Mwilavi
Alisema “tunapotafuta viongozi wa kuchaguliwa tusiangalie sana wanaopendwa na chama, tuangalie mtazamo wa watu wa nje kuhusu watu tunaowapendekeza,” alisema.

Alisema CCM ina hazina ya watu wenye sifa za uongozi lakini wanakatishwa tamaa na lugha za kuchafuana na akawaomba makamanda wa vijana watoe ushauri kwa vijana wenye tabia hizo.

“Makamanda wa UVCCM mna majukumu mengi ya kukisaidia chama kiendelee kuongoza dola, mojawapo ni kuwashauri vijana kwa dhati kabisa waunge mkono CCM na viongozi wake,” alisema.

Alitaja jukumu lingine la makamanda na mlezi wa chipukizi kuwa ni kuhakikisha vijana wanajiandikisha katika dafatari la wapiga kura na wakati wa uchaguzi wanaichagua CCM.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment