Sunday, 9 February 2014

MTOTO WA DK WILLIAM MGIMWA ASHINDA KURA ZA MAONI ZA CCM, KUWANIA UBUNGE JIMBO LA KALENGA

Godfrey Mgimwa alipokuwa akiimboa kura

Akiponngezwa na wafuasi wake

Akipongezwa
Akitoa neno la shukrani huku wagombea wenzake wakimtazama

GODFREY Mgimwa (32) anaelekea kurithi viatu vya marehemu baba yake, Dk William Mgimwa katika jimbo la Kalenga baada ya juzi kuwashinda kwa kishindo wagombea wengine nane wa kura za maoni za Chama cha Mapinduzi (CCM).

Kura hizo zimepigwa ikiwa ni mwezi mmoja baada ya aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo na Waziri wa Fedha Dk Mgimwa kufariki dunia.

Wajumbe 708 kati ya wajumbe halali 816 wa Mkutano Mkuu wa Jimbo la Kalenga kupitia chama hicho waliwasikiliza na kuwapigia kura wagombea hao katika uchaguzi huo uliofanyika kwenye ukumbi wa shule ya sekondari Mwembetogwa, mjini Iringa.

Zoezi la upigaji kura lilianza majira ya saa tisa alasiri baada ya kila mgombea kupata fursa ya kujieleza na kuomba kura na matokeo yalitangazwa  majira ya saa tatu usiku baada ya uhesabuji kura kukamilika.

Mgimwa anayepigiwa upatu wa kushinda uteuzi wa CCM katika uchaguzi mdogo wa ubunge wa jimbo hilo utakaofanyika Machi 16, mwaka huu, alishinda kwa kuzoa kura 348 za maoni.

Akitangaza matokeo hayo, Msimamizi wa uchaguzi huo, Joseph Muhumba alisema Mgimwa alifuatiwa kwa mbali Mkurugenzi wa Kampuni ya Simu za Mikononi ya Tigo Nyanda za Juu Kusini, Jackson Kiswaga aliyepata kura 170.

Wengine na kura walizoambalia kwenye mabano ni Thomas Mwikuka (2), Edward Mtakimo (3), Bryson Kalinga (7), Williama Pangamila (8), Peter Mtisi (33), Mkuu wa Wilaya ya Pangani Hafsa Mtasiwa (42), na mhandisi Gabriel Kalinga (90).

Kabla ya kura hizo kupigwa minong’ono kutoka kwa baadhi ya wajumbe ziliashiria kuwepo kwa ushindani mkubwa kati ya Kiswaga, Mtasiwa na Kalinga.

Hata hivyo Mgimwa alitumia vyema nafasi aliyopewa kujieleza wakati akiomba kura hali inayoelezwa na wajumbe wengi kubadili upepo katika kura hizo.

Bila kumtaja marehemu baba yake, Mgimwa alisema “mimi ni mwenzenu, mkazi wa Kalenga niliyebahatika kupata elimu nzuri.”

Alisema  baada ya kumaliza elimu ya sekondari ya juu hapa nchini alibahatika kwenda nchini Uingereza alikosoma na kujipatia shahada yake ya kwanza na ya pili katika fani ya biashara na masoko.

“Baada ya kumaliza mwaka 2010 nilirejea nchini na kuajiliwa na benki ya Stanbic makao makuu ninakofanya kazi hadi nakuja kuwaomba mnipigie kura ili niwawakilishe katika uchaguzi mdogo wa jimbo la Kalenga,” alisema.

Alisema kwa kupitia Ilani ya CCM atahakikisha anajikita katika kushughulikia kero zinazowahusu wananchi wa jimbo hilo huku kipaumbele chake kikuu kikiwa ni elimu.

Kabla ya kuwashukuru wajumbe kwa kumchagua katika kura hizo za maoni, wagombea wengine wote walikubali matokeo na kuahidi kushirikiana naye katika hatua zote muhimu zitakazokihakikishia CCM ushindi.

Endapo atapitishwa na vikao vya juu vya CCM, Mgimwa anatarajiwa kumenyana na wagombea wa vyama vingine vya siasa kikiwemo Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kilichotarajia kufanya kura zake za maoni jana Jumapili.

Wakati akifungua mkutano wa kura hizo za maoni, Kaimu Katibu Mkuu wa CCM Mkoa wa Iringa, Hassan Mtenga aliwataka wagombea wa nafasi mbalimbali ndani ya CCM kuwa wamoja mara baada ya kura hizo.

“Uzoefu unaonesha kura za maoni zimekuwa zikikigawa chama  kwenye baadhi ya maeneo, tuachane na dhana ya kutoshindwa katika chaguzi zetu za ndani,” alisema.

Alisema wagombea wakionesha mshikamano baada ya kura za maoni itazidi kukiimarisha chama na kukiweka katika mazingira salama ya kushinda chaguzi zijazo.

Taarifa ilitotolewa na Msimamizi wa Uchaguzi Wilaya ya Iringa, Pudenciana Kisaka inaonesha kwamba Tume ya Taifa ya Uchaguzi imepanga tarehe ya uchaguzi mdogo wa jimbo hilo kuwa ni Machi 16, mwaka huu.

Kwa upande wa wagombea kutoka katika vyama vitakavyoshiriki, alisema fomu za uteuzi zitatolewa Februari 9 hadi 18.

Alisema uteuzi wa wagombea utafanyika Februari 18 na kampeni za uchaguzi huo zitaanza Februari 19 hadi Machi 15mara baada ya uteuzi.

Alisema daftari la wapiga kura litakalotumika katika uchaguzi huo ni lile lililotumika mwaka 2010 linaloonesha jimbo hilo lina wapiga kura zaidi ya 85,000 na akawataka wapiga kura kujitokeza kwa wingi siku itakapofika ili waweze kupata mwakilishi wanayemtaka.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment