Tuesday, 18 February 2014

WATAKAOKACHA VIKAO VYA BUNGE LA KATIBA KUKATWA POSHOMbunge ambaye hatashiriki shughuli za Bunge Maalumu, hatapewa posho maalumu, isipokuwa ataambulia Sh 80,000 za posho ya kawaida.


Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah alitoa ufafanuzi huo jana mjini hapa kwa waandishi wa habari na kusisitiza posho hiyo maalumu ya Sh 220,000  lazima anayelipwa awe ameingia bungeni na kushiriki.


"Analipwa baada ya kuona ameshiriki, asiposhiriki atalipwa Sh 80,000," alisema Dk Kashililah ambaye alikuwa akisahihisha baadhi ya taarifa za vyombo vya habari zilizodai kwamba wabunge wa Bunge Maalumu watalipwa Sh 300,000 kila wanapoingia bungeni na kuongeza kuwa wabunge hao hawana mshahara wala kiinua mgongo.


"Penseli, kalamu, karatasi, akitaka kunywa maji, soda, kuvuta sigara tumesema ile ni posho, inaitwa posho maalumu na siyo posho ya kikao kumfanya afanye kama ofisi. Na zaidi ya hizo mbili, hakuna malipo yoyote;  halipwi mshahara wala kiinua mgongo.


"Sasa kilichoandikwa ni kwamba anapokea laki tatu hii (220,000) ni posho maalumu, mpaka aingie, tuone kaingia, leo kaja, ili tuwe na uhakika ametumia  gari, alipiga simu, anaingia mezani ana karatasi ya kuandikia tunasema basi, wataalamu wanasema kumbe amekuja. 


"Na wanamlipa baada ya kumuona ameshiriki, kuhakikisha kwamba kila aliyeteuliwa anashiriki vikao, na kama hatashiriki, hatalipwa, kwa hiyo laki tatu hatapata, atapata elfu themanini."


Awali, baadhi ya wabunge waliozungumza na gazeti hili walitaka malipo hayo yafafanuliwe kwa ufasaha kuweka sawa umma wa Watanzania unaowanyooshea kidole kuwa wanalipwa fedha nyingi. 


"Gharama za uendeshaji zinazotakiwa kutumika kwa posho hii zingefafanuliwa. Hii shilingi laki tatu, hata mtu akijinyima atatumia Sh 200,000," alisema mmoja wa wabunge hao, Maria Sarungi. 


Sarungi alitoa mfano kwamba wapo wabunge wenye wasaidizi mbalimbali wakiwemo madereva au kwa wabunge wenye ulemavu, lazima wawe na wasaidizi, ambao malipo ni lazima yatokane na posho hiyo. 


"Mimi nimefikia hoteli ya kawaida ambayo gharama yake nimeambiwa ni Sh 70,000, dereva wangu anaishi hoteli ya Sh 25,000, ukiangalia chakula, mafuta ya  gari na mahitaji mengine kwa ajili ya bungeni, gharama yake ni kubwa," alisema Sarungi.


Alisema tatizo lililopo ni utofauti wa kiwango cha maisha, hali ambayo mtu ambaye kipato chake kwa siku hakizidi dola moja, ni rahisi kushtuka kwa kusikia kwamba wabunge wanalipwa posho hiyo. 


Wengine ambao hawakutaka kuandikwa majina yao, walisema posho hiyo ya Sh 300,000 ikiangaliwa kwa maana ya wabunge wenye uwezo, jamii inaweza ikaona ni kubwa. 


"Lakini jamii inabidi ikumbuke katika Bunge hili, kuna watu wametoka vijijini na wengine ndiyo kwanza wamefungulia akaunti hapa Dodoma. Ukisema wabunge walipwe Sh 100,000 kwa siku na huyo mbunge akiwemo, unatarajia ataishije hapa mjini," alisema mbunge mwingine ambaye hakutaka kutajwa jina. Aliendelea kusema, "wapo ambao hata usipowapa Sh 300,000 wataishi na watashiriki Bunge kama kawaida. Lakini huyo asiye na mshahara popote, ataweza? Hata teksi atashindwa kulipia."

Reactions:

0 comments:

Post a Comment