Wednesday, 19 February 2014

KIWANDA CHA PINDA CHATELEKEZWA

Waziri Mkuu Mizengo Pinda akiteta jambo na Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Abdalla kigoda
KIWANDA cha kusindika matunda cha Madeke kilichozinduliwa miezi saba iliyopita na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kinaelekea kufa baada ya kukosa fedha za uendeshaji.

Wakulima wa wilaya ya Njombe kilipo kiwanda hicho wameeleza masikitiko yao wakisema hali hiyo itarudisha nyuma mwamko wao wa uzalishaji wa matunda.

Mmoja wa wakulima hao, Saimoni Kyelula alisema kufa kwa kiwanda hicho kabla ya kuanza uzalishaji kumeporomosha bei ya matunda wanayozalisha.

“Wengi tulianza kulima nanasi baada ya kiwanda hiki kuzinduliwa, hivisasa tunalazimika kuuza kwa bei ya hasara yA sh 200 kwa nanasi moja ili kuepuka hasara ya kuozea shambani,” alisema.

Mkulima huyo mwenye shamba la ukubwa wa hekta tano alisema “sifikirii kama nitalima matunda msimu ujao wa kilimo kwasababu mategemeo yangu yameishia kupata hasara.”

Pinda alizindua kiwanda hicho Julai 10, 2013 kikiwa kimeanzishwa kwa lengo kuwawezesha wakulima kuongeza thamani ya matunda wanayozalisha kwa kuyasindika.

Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Madeke, Method Haule alisema kilijengwa kwa zaidi ya Sh Milioni 109.3.

Alisema wakati serikali ilitoa Sh Milioni 100, wananchi walichangia nguvu kazi yenye thamani ya Sh Milioni 9.3.

Alisema serikali imeshindwa kukiendesha kiwanda hicho kinachotafutiwa mbia wa kushirikiana naye.

Haule alisema kama kiwanda hicho kingefanya kazi kama ilivyokusudiwa kingesaidia kuongeza ajira kwa wananchi wa kijiji hicho.

Kijiji cha Madeke kipo katika kata ya Mfriga mpakani na mkoa wa Morogoro na husifika kwa kilimo kutokana na kuwa na ardhi yenye rutuba isiyohitaji mbolea.

Wakazi wa kijiji hicho huzalisha mazao mbalimbali ya chakula na biashara, huku zao kuu la biashara likiwa ni nanasi.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment