Sunday, 2 February 2014

KISWAGA, MTASIWA WAAPISHWA KUSHIKA NAFASI NYETI ZA UVCCCM WILAYA YA IRINGA


Kiswaga akiapa mbele ya Kamanda wa UVCCM Mkoa wa Iringa, Salim Asas kuitumikia UVCCM Wilaya ya Iringa
Mtasiwa akila kiapo cha kuitumiakia UVVCM Wilaya ya Iringa
JACKSON Kiswaga, mdau wa maendeleo wa jimbo la Kelanga, mkoani Iringa ameapishwa kuwa Mlezi wa Chipukizi wa Wilaya ya Iringa kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM).

Ameapishwa juzi, wakati wananchi wa jimbo hilo wakisubiri kwa hamu kusikia ni lini jimbo hilo litafanya uchaguzi mdogo baada ya aliyekuwa mbunge wake, Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa kufariki dunia.

Kiapo chake kilifuatiwa na kiapo cha Kamanda mpya wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Wilaya ya Iringa, Afsa Mtasiwa.

Mtasiwa ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Pangani anachukua nafasi hiyo baada ya kuachwa wazi na mfanyabishara maarufu wa mjini Iringa, Arif Abri.

Vikao vya Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Iringa Vijijini vilivyofanyika hivi karibuni, ndivyo vilivyomteua Kiswaga na Mtasiwa kushika nyadhifa hizo.

Alikuwa ni Kamanda wa UVCCM Mkoa wa Iringa, Salim Asas aliyemlisha kiapo mlezi huyo wa chipukizi na baadaye kamanda huyo wa UVCCM wilaya, kwenye hafla fupi iliyofanyika katika kijiji cha Kalenga.

Akila kiapo cha kukubali uteuzi huo, Kiswaga aliyekuwa akishangiliwa na wakazi wa kijiji hicho alisema “ninaahidi nitakuwa mwaminifu kwa umoja wa viajana wa CCM na CCM, nitaendelea kutii itikadi na imani ya CCM, ninaahidi kuwatumikia vijana wa CCM bila ubaguzi wowote ili wajiimarishe kisiasa na kiuchumi kwa mujibu wa kanuni na katiba ya chama na mila na desturi za watanzania,”

Akiendelea alisema “Ninaahidi kushirikiana na vijana wenzangu kuwaongoza ili wajielimishe kwa bidii na waipende nchi kwa moyo wa kizalendo; naahidi kushirikiana na vijana wote wapenda maendeleo katika nchi yetu kwa hali na mali ili kudumisha historia ya nchi yetu ya amani na mshikamano, Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Afrika kidumu Chama cha Mapinduzi.”

Kiapo kama hicho kilirudiwa na Mtasiwa ambaye katika nasaha zake alisema atatumia maarifa na nguvu zake zote kuhakikisha kwamba umoja huo unakuwa na nguvu kubwa kisiasa.

“Kazi hii haitanishinda,  mimi ni mama, mimi ni mlezi nitawalea vijana wangu; nimechukua dhamana yenu nitawalipa fadhila,” alisema.

Naye Mlezi wa Chipukizi alisema katika kipindi chake cha ulezi atahakikisha anaimarisha shughuli za uchumi wa vijana.

“Tutakaa na kupanga mipango mbalimbali ya kiuchumi ili kuwaondoa katika akili tegemezi ili wajue kujitegemea, kwa kipindi kifupi nimeona mapungufu mengi, tutayaziba ili vijana wengine waje wajifunze kwetu,” alisema.

Katika kutekeleza majukumu yake ya kuimarisha UVCCM wilayani humo, Kiswaga alitoa pikipiki mpya itakayowasaidia kutekeleza majukumu yao ya kikazi ya kila siku.


Kiswaga (mwenye taji la maua shingoni) akimkabidhi pikipiki Mwenyekiti wa Chipukizi Wilaya ya Iringa, Mwilavi, huku viongozi wengine wakishuhudia
Naye Kamanda wa UVCCM Mkoa wa Iringa, Salim Asas alichangia Sh Milioni 3 kwa umoja huo ili uzitumie kujiimarisha kiuchumi.

“Tusionekane makamanda gwanda tu, ni lazima tuoneshe kwa vitendo namna tutakavyousaidia umoja huu kuwa na nguvu kubwa ya kisiasa pamoja na kiuchumi,” alisema.

Aliwataka viongozi hao wateule kufanya kazi ya ziada itakayowavutia vijana wengi zaidi kujiunga na chama hicho imara nchini.  

Asas akitoa ahadi ya kuchangia Sh Milioni 3 kwa UVCCM wilaya ya Iringa

Reactions:

0 comments:

Post a Comment