Tuesday, 4 February 2014

KINANA ATAJA SIFA ZA MGOMBEA UBUNGE KALENGA NA KUWAPONDA CHADEMA KWA KUSHINDWA KUCHANGIA SHUGHULI ZA MAENDELEO YA WANANCHI

Kinana akihutubia wananchi wa Ifunda, jimbo la Kalenga mkoani Iringa
KATIBU Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana ametangaza sifa za mgombea ubunge atakayerithi jimbo lililoachwa wazi na aliyekuwa Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa.

Kabla ya kifo chake, Dk Mgimwa alikuwa mbunge wa jimbo la Kalenga, wilayani Iringa mkoani Iringa.

Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara juzi na mamia ya wakazi wa kata ya Ifunda katika jimbo hilo la Kalenga, Kinana alisema “msichague mbunge anayetafuta cheo ili apate gari na marupurupu ya ubunge.”

Akizitaja sifa za mrithi wa Dk Mgimwa, alisema wananchi wanataka mbunge atakayekuwa mtumishi wa wananchi badala ya kuwa mtukufu.

“Ni muhimu mbunge mtakayemchagua awe yule atakayeweza kuvaa viatu vya Dk Mgimwa, awe mtaratibu,muungwana, mnyenyekevu na mchapa kazi mwenye weledi, uzalendo na uadilifu,” alisema.

Alisema wana Kalenga wanatakiwa kuchagua mbunge msikivu kwa watu na atakaye kuwa tayari kumalia ahadi za maendeleo zilizoahidiwa na marehemu Dk Mgimwa.
 
Baadhi ya wananchi walioshiriki
Wengine wakimsikiliza kwa makini katibu huyo 
“Nina wahakikishieni CCM ina hazina kubwa ya watu wenye sifa kama alizokuwa nazo Dk Mgimwa. Muda ukifika tutawaletea mgombea mwenye sifa kama hizo,” alisema.

Aliwataka wananchi wa jimbo hilo kuachana na wapinzani kwa kuwa wamebaki na kazi kubwa tatu za kuitisha mikutano na maandamano, kukejeli na kutukana watu na kisha kuondoka bila kuchangia shughuli mbalimbali za maendeleo zinazofanywa na wananchi na serikali yao.

“Wako tayari kutumia zaidi ya Sh Milioni 200, kuwatimlia vumbi kwa kutumia helkopta zao, lakini hawawezi kuchangia hata trip moja ya tofali na mawe kwa ajili ya shule mnazojenga au mabomba kwa ajili ya miradi ya maji,” alisema.

Aliwataka wananchi wawaulize Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwanini watumie mamilioni ya fedha kufanya oparesheni ambazo hazichangii maendeleo ya miradi ya wananchi.

“Wakija tena kabla hawajahutubia wasomeeni risala za matatizo yenu na waaulizeni wao wanachangia nini; wasijifanye watu wa mazingaombwe wanaosubiri mpaka waingie Ikulu ndio watende, mbona ninyi mnachangia shughuli zenu za maendeleo kwanini wao wasiwachangie?” alisema.

Alisema katika majimbo yao, wapinzani hao wamekuwa wakijivunia kazi za maendeleo zinazofanywa na serikali ya CCM.

“Mfano leo wanaona serikali ya CCM inajenga barabara za lami, zahanati na shule kila mahali, katika majimbo yao wanasema wamejenga wao. Lakini miradi hiyo ikiharibika hawachangii ili kuikarabati na mkiwauliza watakana kauli zao na kusema hiyo ni miradi ya CCM; wanawafanyia porojo na mazingaombwe,” alisema.

Alisema duniani kote hakuna serikali inayoweza kuleta maendeleo kwa wananchi wake bila kushirikisha nguvu za wadau wake wa maendeleo na wananchi kwa ujumla wao.

“Sisi CCM kazi yetu ni kutenda; tunajua wananchi mnataka barabara, maji, huduma bora za afya, elimu, umeme na mengine mengi; kwa kupitia Ilani ya CCM, serikali kwa kushirikiana nanyi inatekeleza hayo,” alisema.

Alisema moja ya kero kubwa inayowasibu wananchi wa Ifunda na ambayo iliahidiwa na Dk Mgimwa kutekelezwa kabla ya 2016, ni maji.

“Hii ni ahadi itakayotekelezwa na serikali na nimekwishaambiwa serikali inakusudia kutumia sh bilioni tano kumaliza tatizo la maji Ifunda; niwahakikishie huduma hiyo ya maji itakuja kwakuwa kazi ya serikali ya CCM ni kushughulikia kero za wananchi,” alisema.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment