Wednesday, 5 February 2014

KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA KUPAMBANA NA UKIMWI YATEMBELEA KITUO CHA TARWOC IRINGA


Lediana Mng'ong'o

Wajumbe na kamati hiyo

Wakikagua kituo hicho

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Kupambana na Ukimwi imeipongeza taasisi ya Maendeleo ya Wanawake na Watoto Vijijini (TARWOC) kwa kutekeleza mpango wa kupambana na ukatili wa kijinsia wilayani Iringa.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Lediana Mng’ong’o alisema “pamoja na changamoto mlizonazo mnaonesha kutimiza wajibue wenu.”

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mipango ya taasisi hiyo, Meneja wa Kituo, Pendo Luoga alisema kuanzia mwaka 2011 mpaka sasa, wamefanikiwa kutoa elimu juu ya ukatili wa kijinsia kwa watu wapatao 29,476.

Alisema kati yao wanaume ni 11,580 sawa na asilimia 39 na wanawake ni 17,896 sawa na asilimia 61.

Alisema mradi huo unaendeshwa katika kata zote 16 za manispaa ya Iringa na kata nne za halmashauri ya wilaya ya Iringa.

Alizitaja huduma zinazotolewa na kituo chao kuwa ni pamoja na ushauri, usuluhishi, malazi, chakula, mavazi na rufaa.

“Hiki ni kituo cha kujihifadhi kwa muda, kinachotetekeza mradi wa kupambana na ukatili wa kijinsia kwa kutoa huduma mbalimbali kwa waathirika wa vitendo hivyo na kuelimisha jamii kuu ya masuala hayo.

Alisema tangu kuanza kwa mradi huo, uelewa wa jamii katika masuala ya kupinga ukatili wa kijinsia na uhusiano wa vitendo vya ukatili wa kijinsia na maambukizi ya VVU/Ukimwi umeongezeka.

Alisema idadi ya wananchi wanaotoa taarifa ya matukio ya ukatili wa kijinsia kama ubakaji, kulawiti na vipigo imeongezeka kutoka wateja 49 katika kipindi cha miezi mitatu kwa mwaka 2011 na kufikia wastani wa wateja 100 kwa kipindi cha kila miezi mitatu mwaka jana.

Alisema mradi huo umewezesha pia kupungua kwa idadi ya watoto wa mitaani kutokana na elimu, ushauri na upatanishi wa wanandoa au wanafamilia wanaoutoa.

Kutokana na mafanikio hayo, alisema shirika limesaini mkataba wa makubaliano na halmashauri ya manispaa ya Iringa na kupewa kiwanja cha ukubwa wa mita za mraba 4,000 ili wajenge kituo badala ya kuendelea kupanga.

Kamati hiyo ya bunge ilikuwa mkoani hapa na kutembelea miradi mbalimbali inayolenga kupambana na maambukizi ya VVU/Ukimwi.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment