Wednesday, 19 February 2014

JAJI MFAWIDHI MAHAKAMA KUU KANDA YA IRINGA AWATAKA POLISI KUFUATA TARATIBU ZA MAHAKAMA

Jaji Mary Shangali akikagua gwaride la askari Polisi siku ya sheria nchini

JAJI wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa, Mary Shangali amelaani vikali vitendo vya unyanyasaji vinavyofanywa na jeshi la Polisi kwa wanahabari wa mjini Iringa.

Pamoja na laana hiyo amewataka askari Polisi wawapo katika mahakama yake wazingatie taratibu za mahakama.

Aliyasema hayo mara baada ya kupokea taarifa ya kusikitisha inayowahusisha baadhi ya askari Polisi bila ridhaa yake kumtoa nje ya mahakama na kumfikisha katika kituo cha Polisi mmoja wa wanahabari wanaofanya kazi zao mjini Iringa.

Mwanahabari huyo Frank Leonard, alifanyiwa hayo kwa kile kilichoelezwa na askari hao kwamba alikuwa akipiga picha wakati mahakama hiyo ikiendelea.

Ilikuwa wakati jaji huyo akisikiliza kesi ya mauaji ya mwandishi wa Channel Ten, Daudi Mwangosi inayomkabili aliyekuwa askari wa jeshi hilo, Pasificus Cleophace Simoni.

Kesi hiyo ilianza kusikilizwa kwa mara ya kwanza mahakamani hapo, Februari 13 kwa kile kilicholezwa na upande wa mashtaka kwamba uchunguzi wake umakamilika.

“Wameitendea kosa mahakama hii na wamtendea kosa mwanahabari huyo; kazi waliyofanya siyo yao , inakiuka taratibu za mahakama,” alisema.

Alisema kama kweli mwandishi huyo alikuwa akipiga picha na kuhatarisha mwenendo wa shughuli za mahakama, askari hao walichopaswa kufanya nikuandika memo kwake ili achukue hatua.

“Hawatakiwi na hawastahili kuingilia kazi nazotakiwa kufanya mimi au viongozi wengine wa mahakama wakati mahakama ikiendelea” alisema.

Alisema mahakama inafanya kazi na wanahabari na itaendelea kufanya nao kazi huku akiwasihi Polisi kuacha kuwabugudhi.


“Siku nyingine mkija na mkaona kuna dalili ya kufanyiwa kama haya aliyofanyiwa mwenzenu tunaomba mtoe taarifa kwangu au kwa msajili wa mahakama ili tuchukua hatua,” alisema.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment