Wednesday, 12 February 2014

GREEN CITY YATOA MSAADA WA MIFUKO 35 YA SARUJI KATA YA MAZOMBE, KILOLO

Professa Msolla (kulia) akipokea fedha kutoka kwa Mwakilishi wa kampuni ya Green City, Amoni Shaidi kwa ajili ya kununua mifuko 35 ya saruji ili kufanikisha ujenzi wa ofisi ya kata ya Mazombe

Katika picha ya pamoja nje ya ofisi hiyo ya kata

Jengo la Ofisi ya Kata ya Mazombe linavyoonekana

KAMPUNI ya Green City ya Dar es Salaam imetoa msaada wa mifuko 35 ya saruji ili kufanikisha ujenzi wa ofisi ya kata ya Mazombe wilayani Kilolo. 

Kampuni hiyo inayojishughulisha na ujenzi wa vituo vya maegesho ya magari makubwa, mabasi na madogo nchini ilikabidhi msaada huo kwa Mbunge wa Jimbo la Kilolo, Profesa Peter Msolla.

Moja ya vituo hivyo vitakavyokuwa na maduka, hoteli,  huduma za kibenki, vituo vya mafuta na nyumba za kulala wageni kitajengwa Mazombe huku vingine vikijengwa Melela Morogoro na Igulusi mkoani Mbeya.

Kijiji cha Mazombe kipo, wilayani Kilolo barabara ya Iringa Dar es Salaam karibu kabisa na mji mdogo wa Ilula.

Akikabidhi msaada huo kwa mbunge huyo, Mwakilishi wa kampuni hiyo, Amon Shaidi alisema utawezesha jengo lote kupigwa sakafu na plasta.

Ikiwa ni shukrani kwa kijiji cha Mazombe kuwapatia ardhi kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho cha maegesho ya magari, Shaidi alisema misaada zaidi kwa ajili ya kufanikisha ujenzi wa ofisi ya kata hiyo itatolewa sambamba na misaada mingine kwa jamii katika sekta ya elimu, afya na zingine za maendeleo.

“Tumetoa sementi kama moja ya ahadi yetu ya kushirikiana na wananchi wa kata ya Mazombe kufikia malengo yao ya kimaendeleo, misaada mingi zaidi ikiwemo rangi kwa ajili ya jengo hili inakuja,” alisema.

Akipokea msaada huo Mbunge wa Kilolo ambaye pia ni Mshauri Mkuu wa Makamu wa Rais, Profesa Msolla alisema “wawekezaji wanaoshiriki shughuli za kijamii wanaongeza uhusiano na jamii inayowazunguka.” Alisema.

Alisema kuingia kwa kampuni hiyo katika kijiji cha Mazombe kutaongeza fursa kwa wakazi wa kata hiyo.

Alizitaja fursa hizo kuwa ni pamoja na ajira zitakazosaidia kubadili maisha ya wenyeji wa kata ya Mazombe.

“Kwa kupitia kituo hicho wapo watakaoajiriwa lakini kwa upande wa huduma mtajihakikishia soko la bidhaa mnazozalisha mashambani kwasababu mtauza vyakula manavyozalisha kwa matumizi ya hoteli zitakazojengwa,” alisema.

Alisema ujio wa kampuni hiyo utajenga jina la Mazombe kwa kuwa kituo kitakachojengwa kitakuwa kikubwa kitakachotoa huduma kwa wasafirishaji wa ndani na nje ya nchi.


Katika mipango yake ya kushirikiana na wananchi wa Mazombe, aliiomba kampuni hiyo isaidie kuboresha miundombinu ya upatikanaji wa maji katika kijiji hicho na vijiji vingine jirani.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment