Kwa desturi ya kabila la wahehe
mtoto wa kike tangu anapozaliwa anahesabiwa kuwa ni mpita njia katika familia
yake (kwamba ni lazima ataolewa hapo baadae) na atakwenda kuendeleza ukoo
mwingine hivyo hana haja ya kuhesabiwa urithi nyumbani kwa baba yake.
Kama hiyo haitoshi, pia anapoolewa
mume ndiye anakuwa mmiliki wa ardhi hata kama mwanamke ndiye ametoa hela za
ununuzi wa kiwanja ama shamba.
Hakuna sababu za msingi katika hilo
lakini wanaume wengi pengine kwa sababu wao ndio wamesoma shule, ama mfumo dume
wamekuwa wakiandikisha majina yao tu katika hati za umiliki na kama mwanamke
ana watoto atamwandikisha mtoto wa kiume kama ndiye mrithi.
Yapo madai kuwa maamuzi hayo
yanatokana na endapo mwanamume atafariki basi yule mwanamke anaweza kuolewa na
mwanaume mwingine na mali ikapotea.
Jambo la kusikitisha zaidi ni pale
mwanamke anapofariki kwani kwa mila na desturi mwanamke haruhusiwi kuzikwa
nyumbani alikozaliwa (kwao) mpaka mume aidhinishe ardhi ambayo mwanamke huyo
atazikwa.
Mchungaji Agness Kulanga wa kanisa
la KKKT anasema “ zipo kesi nyingi tu ambazo tumeitwa tukasuluhishe katika
misiba kutokana na mzozo wa mahala pa kuzika hasa mwanamke anapofariki kwa
sababu mwanaume hakumaliza mahari au alimchukua binti kinyume na taratibu.
“Hii ni mila inayomdhalilisha
mwanamke kwani anayedhalilika ni yule mwanamke aliyefariki huu ni ukatili kwani
hakuna mwanaume ambaye anafanyiwa kitendo kama hicho”
Kuhusu umiliki wa ardhi anasema hata
Biblia imeruhusu watu wote kumiliki ardhi katika Isaya 60:21 watu wako
nao watakuwa wenye haki wote, nao watairithi nchi milele: Hivyo kumnyima
mwanamke kumiliki ardhi ni kumkandamiza kijinsia .
Diwani wa kata ya Miyomboni katika
manispaa ya Iringa Bi Jesca Msambatavangu anasema kuna haja ya wanawake kuamka
na kuanza kutafuta ardhi ya kwao binafsi bila ya kujali kama wameolewa au la .
“Wanawake wanatakiwa kuamka na
kuunda vikundi vya pamoja ili waweze kununua ardhi kidogo kidogo kwani wengi
wanatamani kununua ardhi ila wanashindwa kutokana na kipato chao kuwa kidogo
hivyo wakijiunga kwa pamoja wanaweza kununua shamba kisha baadae wakagawana hii
itawasaidia wanawake kumiliki ardhi mmoja mmoja”anasisitiza Bi Msambatavangu
Bi Lucy Mgoba mkazi wa kitwiru (38)
manispaa ya Iringa baada ya kutelekezwa na mume wake na watoto wawili
miaka miaka mitano iliyopita, aliamua kujipanga na kukabiliana na tatizo
lililompata kwa kuanza kufanya biashara ndogondogo ya chakula na kujiunga na
vikundi vya mikopo midogo midogo huku akijibanza na watoto wake nyumbani kwa
mama yake.
Akiwa huko alianza kuweka
akiba kwa kila pesa ambazo alikuwa anazipata na kujinyima anasa ili
watoto wake wapate chakula na mahitaji ya shule.
Anasema alikuwa anaishi na mume wake
Dar es salaam baada ya maisha kuwa magumu wakaamua kurudi nyumbani Iringa
ambako alimtelekeza.
Anashukuru Mungu kwa sasa biashara
zake zimemuwezesha kununua shamba nusu ekari na kuanza maandalizi ya
ujenzi wa nyumba.
Pamoja na kuwa na nyumba ya vyumba
vitano anasema tatizo lingine wanalokutano nalo wanawake katika umiliki wa
ardhi ni pamoja na uelewa mdogo wa sheria ya umiliki wa ardhi pamoja na mirathi
kwa wanawake walio wengi.
Hili lipo wazi zaidi kwa
kuangalia yaliyomsibu Bi Tumaini Anelea Mgege (28) .
Mwanamke huyu ambaye alijenga nyumba
ya vyumba vitatu baada ya kununua kiwanja eneo la Mtwivila kwa fedha ambayo
ilitokana na kuuza ubuyu na maandazi shule ya msingi iliyo jirani na nyumba
aliyokuwa amepanga, anasema aliporwa nyumba hiyo baada ya kumkaribisha mume
wake waishi pamoja.
Alisema baada ya kuhamia katika
nyumba hiyo mgogoro mkubwa ukaikumba ndoa yake jambo lililomfanya yeye kutoroka
kwenda kwa dada yake: Kwa bahati mbaya kabla hajarudi nyumbani kwake, mume wake
akapata ajali katika basi ambalo alikuwa ni kondakta akafa na hapo ndipo
dhuluma ilipoanza dhidi yake.
Bi Tumaini anasema alipopata taarifa
ya kifo akatoka kwa dada yake kwenda Ifunda kwa wazazi wa mume wake ambako mama
mkwe alimpiga kwa madai ya kuwa yeye ndiye aliye muua mume wake kwa ushirikina.
Pamoja na ndugu zake kumtetea
ilishindikana kushiriki hata mazishi ya mume wake.
Msiba ulipoisha alirejea nyumbani
kwake Mtwivila na kupigwa butwaa pale alipokuta nyumba ile imewekwa wapangaji
walioingizwa na wakwe zake.
Baada ya kuona mambo ni magumu
aliomba msaada kutoka kwa viongozi wa dini ambao walimpeleka ofisi za
serikali ya mtaa ili kuweza kupata msaada wa sheria na baada ya upande wa pili
kuitwa ikaamuliwa ile nyumba iuzwe kwa shilingi laki mbili na pesa
zigawanywe kwa wote.
Kwa kutojua sheria alikubaliana nao
kwa shingo upande huku akijua kabisa kuwa ardhi na nyumba ni mali yake
kiuhalali na pesa ambayo nyumba hiyo inauzwa haifikii hata nusu ya gharama
ambayo imetumika kujengea.
Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa
ambaye hakuwa tayari kutaja jina lake alisema kwa ufupi kwamba mwanamke huyo ni
kweli alifika katika ofisi hiyo na walita baraza wakamsikiliza na akasaini
mkataba wa mauzo na kudai kuwa kama yeye angejua kama anaonewa angekata rufaa
wala asingeruhusu nyumba kuuzwa .
Kwa upande wake Bi Tumaini anasema
kutokana na wakwe zake kumtishia kuwa wangeondoa uhai wake endapo angechukua
hatua nyingine ya kuwafikisha mahakamani aliogopa na ndiyo sababu inaliyomfanya
akubaliane nao na huku akijua kuwa mnunuzi wa nyumba hiyo ni ndugu wa mume na
ndiyo sababu wametaja bei hiyo ndogo.
Wanaume waliohojiwa kuhusu umiliki
wa ardhi kwa wanawake hofu yao inaonekana kuzidiwa na fikra mgando zenye
desturi ambazo ni ngumu kuzifuta katika ubongo wao.
Bw Robert Kinisa anasema
hakuna haja ya mke wake kuwa na ardhi yake pekee ama kumwandikisha katika
urithi kwani ardhi aliyonayo ni yao wote japokuwa hati miliki zina jina
lake huku urithi akiwa amemwandikisha mtoto wao wa kwanza wa kiume .
“Hata nikifa leo mtoto wangu
atamtunza mama yake lakini hati ikiandikwa jina la mke wangu pengine nikifa
ataolewa na mwanaume mwingine na kuishi naye nyumbani kwangu na kuwanyima haki
watoto wangu. “Lakini pia hofu nyingine mwanamke akijua umemwandikisha katika
urithi wa ardhi anaweza kukuua ufe haraka ili arithi na wanawake wengine wana
kuwa na kiburi na jeuri mara tu wanapokuwa wanamiliki ardhi.” Alisema.
Mwanasheria Asifiwe Mwanjala anasema
sheria inatamka wazi kwa mwanamke na mwanaume wote wana haki sawa na kwa
masharti yaleyale kumiliki ardhi; na kuwa ardhi kama rasilimali kuu ya kiuchumi
na kijamii inasimamiwa na kuratibiwa na sheia ya ardhi ya mwaka 1999 na sheria
ya ardhi ya vijiji ya mwaka 1999.
Lakini anasema changamoto kubwa si
ukosefu wa elimu ya sheria lakini pia ni kuwa hata wale wanawake wenye uelewa
wakati mwingine wanashindwa kupata haki yao kutokana na kushindwa kulipia
gharama za kuweka mwanasheria na kukosa ushahidi kwani baadhi yao wanapofungua
mashtaka wanashindwa kuwa na uthibitisho wa hati ama kumbukumbu zozote za
kimandishi japo wakati mwingine wanaweza kupata msaada wa mashahidi.
Kuhusu mila potofu anasema kifungu
20(2) cha sheria ya ardhi ya vijiji ya 1999 inakataza matumizi ya kanuni ya
mila kandamizi na kwamba umiliki wa kimila utakuwa batili kama unawanyima
wanawake haki ya kupata umiliki wa ardhi.
Mila potofu ni pamoja na zile
zinazopitishwa na wanafamilia wakati wa urithi ama wakati wa talaka kwani mila
na tamaduni za kihehe si rafiki kwani hazitoi fursa kwa mwanamke kumiliki
ardhi.
Diwani Elizabeth Mpogole
anasema kwanza yeye mwenyewe alikuwa hajui kama sheria inamruhusu kumiliki
ardhi yake binafsi kwani ardhi aliyonayo ni ya mume wake hivyo sasa amepata
mwanga na anadhani ipo haja kuwasilisha hoja katika baraza la halmashauri ili
wanawake wapewe kipaumbele kwenye mgao wa viwanja vinavyouzwa na manispaa .
Vurugu zinaoztokea katika jamii ya
wahehe kuhusu yumiliki wa ardhi ni kinyume na sheria za nchi, kwani Msingi
wa sera ya nchi ya Tanzania 1995 mwanamke anaweza kupata
ardhi kwa njia ya urithi kutoka kwa mume au wazazi wake kama kutakuwepo na
wosia na mwanamke ametajwa katika wasio basi atakuwa na haki ya kurithi.
Kama hakutakuwa na wosia basi katika
mgawanyo wa mirathi mwanamke anayo haki ya kurithi ardhi pia.
Pia Mwanamke anaweza kupata ardhi
kwa kugawiwa na Serikali, anaweza kuomba ardhi katika ardhi ya jumla au ya
kijiji.
Sheria za Tanzania hazimnyimi
mwanamke haki ya ardhi ila mfumo wetu wa kijamii hautoi fursa kwa mwanamke.
Kukabili tatizo hilo ni vyema
kukaanzishwa kampeni kwa wanawake na wanaume kufahamu haki za urithi kwa
mwanamke ili kila mmoja awe katika nafasi nzuri ya kutetea haki za
wanawake wakati wa urithi na katika kuendesha maisha ya kawaida.
0 comments:
Post a Comment