Wednesday, 5 February 2014

CHUO CHA MAENDELEO YA JAMII RUAHA CHALALAMIKIA MGAO WA FEDHA

CHUO cha Maendeleo ya Jamii Ruaha kimelalamikia mgao wa fedha inazokusanya na kuzipeleka hazina kwamba zinafifisha ufanisi wake.
 
Mkuu wa  Chuo, Msigala
Mbele ya wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii na naibu waziri wa maendeleo ya jamii, jinsia na watoto na wa habari, utamaduni na michezo, Mkuu wa chuo hicho, Gerald Msigala alisema kiasi cha fedha wanachorudishiwa ni kidogo.

“Mapato yetu makubwa yanatokana na ada tunazokusanya toka kwa wanafunzi wetu, lakini haturuhusiwi kutumia fedha hizo na badala yake hupelekwa retention account,” alisema.

Alisema mbali na fedha wanazorudishiwa kuwa kidogo, hazirudishwi kwa wakati na hivyo kukwamisha shughuli za uendeshaji na mafunzo.

Akitoa mfano wa msimu wa masomo wa 2013/2014, Msigala alisema chuo kilikusanya zaidi ya Sh Milioni 200 lakini walizorudishiwa baada ya kupeleka kwenye akaunti hiyo ni sh Milioni 76 tu.

“Baadhi ya shughuli ambazo zimekwama kabisa kutoka na ukosefu wa fedha ni pamoja na ukarabati wa ukumbi wa mihadhara, mabweni mawili, nyumba za watumishi, ujenzi wa choo katika ukumbi unaokarabatiwa, ununuzi wa vitabu kwa ajili ya maktaba na ulipaji wa madai mbalimbali ya watumishi.

Akijibu madai hayo Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Pindi Chana alisema serikali italifanyia kazi suala hilo.
 
Dk Pindi Chana, Naibu Waziri Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto
Hata hivyo alisema ni muhimu serikali ikajua makusanyo yote yanayofanywa katika vyuo hivyo ili kuongeza uwajibikaji na uwazi.

Alisema baada ya kujulikana na serikali ni muhimu fedha hizo zikarudi kwa chuo husika kwa muda na kiwango kinachotakiwa.

“Suala la kupitia hazina ni la muhimu sana ili kuondoa hofu ya matumizi mabaya ya fedha za umma, lakini tutaangalia namna ya kuboresha marejesho yake ili zilirudi kwa muda na kiwango kinachotakiwa,” alisema.

Alisema vyuo vya maendeleo ya jamii ni muhimu kwa maendeleo ya Taifa kwakuwa vinafundisha uzalishaji kwahiyo wizara inafanya kila inaloweza kuviimarisha.
 
Wakikagua mazingira ya chuo
“Hivi ni vyuo ambavyo watanzania wengi wanaweza kupeleka watoto wao huko kwasababu gharama zake ni ndogo,” alisema.

Alisema wizara itaviboresha vyuo vya maendeleo ya jamii 55 nchini sambamba na kuuimarisha miundombinu yake.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment