Sunday, 9 February 2014

CHADEMA YAGARAGAZWA CHAGUZI NDOGO ZA UDIWANI MKOANI IRINGA, YAKUBALI MATOKEO

Polisi walikuwepo wakati matokeo hayo yakitangazwa, kuhakikisha uvunjifu wa amani hautokei
wana CCM kata ya Nduli wakifurahia  ushindi
 
MBIO za chaguzi ndogo za udiwani katika kata tatu mkoani Iringa zimehitimishwa kwa Chama cha Mapinduzi (CCM) kukigaragaza vibaya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Mkoa Iringa kata tatu ikiwemo ya Nduli, Mjini Iringa na Ukumbi na Ibumu wilayani Kilolo zilishiriki uchaguzi huo ikiwa ni matokeo ya waliokuwa madiwani wake, wote kupitia CCM kwa nyakati tofauti kufariki dunia.

Katika chaguzi hizo Chadema ilionekana kuwekeza nguvu iliyoshereheshwa na viongozi wake wa kitaifa kwa kupitia kampeni ya M4C Operasheni Pamoja Daima kufanya kampeni katika kata hizo.

Katibu Mkuu wa Chadema Dk Wilbroad Slaa na Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe walifanya kampeni katika kata hizo kwa kutumia helkopta yao wakiwa na viongozi wengine wa kitaifa wa chama hicho.

Pamoja na viongozi hao wabunge kupitia chama hicho, Mchungaji Peter Msigwa na yule wa Viti Maalumu Mkoa wa Iringa, Chiku Abwao waligawana majukumu katika kata hizo.

Wakati Mchungaji Msigwa akifanya kampeni katika kata ya Nduli na mara moja moja katika kata hizo zingine,  Abwao kwa upande wake alikita zaidi katika kata ya Ibumu na Ukumbi.
Katika kampeni zake kata ya Nduli, Mchungaji Msigwa aliahidi kugawa mbolea kwa wananchi wa kituo cha kupigia kura ambacho Chadema ingeongoza kwa kura.

Hata hivyo kati ya vituo tisa vya kata hiyo ya Nduli, Chadema ilifanikiwa kuongoza kwa kura katika kituo kimoja tu cha Mwibata kwa mgombea wake kupata kura103.

Akitangaza matokeo katika kata ya Nduli, Msimamizi wa Uchaguzi, Simba Nyunza alisema kati ya kura zote zilizopigwa, Mgombea wa CCM, Bashir Mtove alipata kura 810 huku Ayubu Mwenda wa Chadema akiambulia kura 491.

Huko wilayani Kilolo matokeo yaliyothibitishwa na mawakala wa CCM yanaonesha chama hicho kimepata ushindi mkubwa.

Katika kata ya Ibumu, mgombea wa CCM Gift Msumule ameibuka kidedea baada ya kupata kura 1,400 huku mgombea wa Chadema, Juli Mpungula akiambulia kura zaidi ya 400.

Katika kata ya Ukumbi, mgombea wa CCM, Hemed Mbena ameshinda kwa kishindo baada ya kuzoa kura 1479 dhidi ya kura 829 alizopata mgombea wa Chadema, Oscar Ndale.  

Katibu wa CCM Manispaa ya Iringa, Hassan Mtenga alisema ushindi huo unatoa mwelekeo mzuri kwa chama chao kurejesha katika chama chake jimbo la Iringa mjini linaloongozwa na Mchungaji Msigwa.

Mtenga ambaye pia ni Kaimu Katibu wa CCM Mkoa wa Iringa alisema watafanya sherehe kubwa kuwapongeza wagombea wao wa kushindi mnono waliopata.

“Sehere hizo zitakwenda sambamba na mikutano mikubwa kwa ajili ya kuwashukuru wananchi kwa kuichagua CCM katika uchaguzi huo,” alisema.

Reactions:

1 comments:

  1. Ni ushindi halali au uchakachuaji huo?

    ReplyDelete