Thursday, 16 January 2014

WAZIRI MKUU KUAMUA UJENZI WA STENDI MPYA YA IRINGA, MEYA AWALAUMU WANASIASA WANAOPANDA MAAMUZI YA KITAALAMU

MAAMUZI ya mwisho ya ujenzi wa stendi mpya ya mabasi yaendayo mikoani katika eneo la Igumbilo, mjini Iringa yapo mikononi mwa Waziri Mkuu hivisasa.

Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Manispaa ya Iringa liliamua kupeleka suala hilo kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda baada ya kuwepo na taarifa kutoka kwa wadau wanaoitaka halmashauri hiyo isitishe ujenzi wa stendi hiyo katika eneo hilo.

Akizungumza na wanahabari hivikaribuni, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk Christine Ishengoma alisema “tumeishauri halmashauri hiyo itafute eneo lingine baada ya kupokea pingamizi la wadau wa mazingira.”
 
Meya wa Manispaa ya Iringa, Amani Mwamwindi
Wadau hao wanapinga kwa kile kinachoonekana inajengwa karibu na kingo za mto Ruaha Mdogo.

Akitetea uamuzi wa halmashauri hiyo Mstahiki Meya wa Manispaa ya Iringa, Amani Mwamwindi alisema “uamuzi wa kujenga stendi katika eneo hilo ulishirikisha watalaamu lakini inashangaza unageuzwa siasa.”

Katika mkutano wake alioufanya mjini Iringa hivikaribuni, Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa alisema “haungi mkono ujenzi wa stendi hiyo katika eneo hilo.”

Msigwa alisema katika kuhalalisha uamuzi wao unaolenga kuharibu mazingira ya mto huo ambao maji yake yanatumiwa kwa shughuli za kibinadamu na wakazi wa manispaa ya Iringa, madiwani wa halmashauri hiyo walikwenda mjini Dodoma na kukutana na Waziri Mkuu ili wamrubuni.

Akidhihirisha jinsi suala la ujenzi wa stendi hiyo linavyopotoshwa na wanasiasa, Mstahiki Meya alisema inajengwa mita 750 kutoka katika kingo za mto huo pamoja na kwamba sheria inataka shughuli za kibadamu zifanyike mita 60 kutoka katika kingo za mto.

Alisema wakati wanasiasa wakilalamikia uamuzi huo, katika eneo la Ipogolo ambako pia mto huo unapita nyumba za makazi na biashara zimejengwa mita 60 kutoka kwenye kingo.

“Tunataka stendi ijengwe hapo kwasababu wataalamu wamethibitisha hakutakuwa na madhara; hizi ni jitihada za CCM za kuwaletea wananchi wa mjini Iringa maendeleo, tunataka kupanua mji na shughuli zake tukiwa katika mikakati ya kuwa Jiji,” alisema.

Kwa mujibu wa mstahiki meya, Tathimini ya athari za kimazingira katika eneo hilo ilifanywa na Mtaalamu Mshauri wa Mazingira (CONSULTANT) aitwaye Arms on Environment Ltd wa Dar es Salaam.

Alisema baada ya tathimini hiyo kuridhia stendi hiyo ijengwe katika eneo hilo, walipata hati ya ya ujenziwake kuwa ni Na.EC/E15/584 iliyotolewa Juni 15, mwaka jana

Kwa mujibu wa Mhandisi wa halmshauri hiyo, Mashaka Luhamba, mpaka kukamilika kwake stendi hiyo itagharimu zaidi ya Sh Bilioni 4.


Fedha hizo zitatolewa kupitia Programu ya Uendelezaji Miji inayosimamia na Ofisi ya Waziri Mkuu kwa ufadhili wa Benki ya Dunia.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment