Thursday, 30 January 2014

TANROADS KUTUMIA KAMERA ZA CCTV KUWABAINI WANAOTOA NA KUPOKEA RUSHWA

 
Meneja wa Tanroads paulo Lyakurwa akitoa taarifa hiyo
KATIKA kupambamba na vitendo vya rushwa kwenye mizani ya kupimia magari makubwa, Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) mkoa wa Iringa imefunga kamera  aina ya CCTV ili zisaidie kuwaumbua watumishi wenye tabia hiyo.

Meneja wa Tanroads mkoa wa Iringa, Paulo Lyakurwa alisema kwa kuanzia kamera hizo zimefungwa kwenye mzani wa kisasa unaotumia teknolojia ya dijitali wa Wenda;mzani huo upo Tanangozi, Iringa Vijijini barabara ya Iringa Mbeya.

Akitoa taarifa hiyo kwenye kikao cha Bodi ya Barabara jana, Lyakurwa alisema kamera hizo zimegharimu zaidi ya Sh Milioni 30.

Alisema kwa kupitia kamera hizo, magari yote makubwa yanayopita katika barabara hiyo yatapigwa picha kabla na baada ya kupima mzani.

“Hata yale yatakayokuwa yakiruhusiwa kupita bila kupima uzito yatabainika kupitia kamera hizo zitakzokuwa zikiwapiga picha watumishi wa mizani na mambo yao wanayofanya,” alisema.

Alisema rushwa ni changamoto kubwa kwenye mizani inayochangia kwa kiasi kikubwa kuharibu barabara na uchumi wa nchi.

“Ni hatari kuendelea na watumishi wa mizani wanachukua rushwa na kuruhusu magari yaliyozidisha uzito kuendelea na safari,” alisema.

Kwa kupitia kamera hizo ambazo zimefungwa kila kona ya eneo hilo la mizani, alisema Tanroads itaweza  kubaini kinachofanywa na watumishi wake katika kuhujumu dhana nzima ya kudhibiti magari yanayozidisha uzito.

Akichangia hoja, Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoa wa Iringa, Emma Kuhanga alisema kilichofanywa na Tanroads ni kizuri lakini kinatakiwa kusimamiwa kwa umakini.

“Lazima muwe makini maana fitina zinaweza kutumika kuwahukumu watu vibaya kwa kutumia kamera hizo; hakuna dhambi watumishi na wateja wao kusalimiana kwa kushikana mikono, mazingira hayo yasije yakatafsiriwa kama kitendo cha kutoa na kupokea rushwa,” alisema.

Alisema rushwa ni tukio linalofanywa kwa makubaliano ya pande mbili zinazotaka kuvunja sheria, CCTV kamera zinaweza kusaidia kubaini hilo lakini ni muhimu pia katika mazingira yenye hofu ya rushwa kukawepo na watu wanaoweza kutoa ushahidi.

Aliitaka Tanroads isisubiri taarifa zinazorekodiwa na kamera hizo ili iwawajibishwe watumishi wasio waaminifu.

“Msisubiri kamera, kama kuna watumishi wenye tabia zinazoathiri ufanisi wa idara hiyo ya mizani waondoeni kazini,” alisema.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment