Thursday, 23 January 2014

MCHUNGAJI MSIGWA AKABIDHI HATMA YA UBUNGE WAKE 2015 KWA WAPIGA KURA


MBUNGE wa Jimbo la Iringa Mjini Mchungaji Peter Msigwa (Chadema) amesema  kurudi kwake bungeni katika Uchaguzi Mkuu wa 2015 kutategemea maamuzi ya wapiga kura wa jimbo la Iringa Mjini.

Akihojiwa na Redio Nuru FM hivikaribuni Mchungaji Msigwa alisema “ kurudi kwangu bungeni kutategemea maamuzi ya wananchi na nitaheshimu uamuzi wao.”

Aliyasema hayo baada ya mmoja wa wauliza maswali aliyejitambulisha kwa jina la Jackson kuonesha hofu endapo mbunge huyo atachaguliwa kwa mara nyingine tena kushika wadhifa huo.

“Hivi Mchungaji Msigwa unadhani kweli wananchi wa jimbo la Iringa Mjini watakuchagua tena uwe mbunge wao, nina wasiwasi na hilo?” aliuliza.

Katika majibu yake kwa muuliza swali Mchungaji Msigwa alisema ubunge wake utategemea maamuzi ya wapiga kura.

Hata hivyo alisema kwa nafasi aliyonayo anaendelea kufanya kazi ya kuwawakilisha wananchi katika chombo muhimu cha kutunga sheria na kuikosoa serikali ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ili iwaletee wananchi maendeleo wanayoyataka.

Wakati huo huo, Mchungaji Msigwa ameendelea na msimamo wake wa kupinga ujenzi wa stendi mpya ya mabasi katika eneo la Igumbilo.

“Nilikutana na Waziri Mkuu na nikamueleza athari za kujengwa kwa stendi hiyo katika eneo hilo; wana mazingira wamepinga na mimi napinga; ushauri wangu litafutwe eneo lingine la kujenga stendi hiyo,” alisema.

Alipoulizwa ni wapi anadhani panafaa kwa ujenzi wa stendi hiyo, Mchungaji Msigwa alisema “hilo sio suala la Msigwa pekee yake, linahitaji maamuzi ya pamoja kwahiyo kukiwa na fursa hiyo tutashauriana kwa pamoja.”

Taarifa iliyotolewa na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Iringa, Amani Mwamwindi hivikaribuni inaonesha kwamba manispaa hiyo inasubiri maamuzi ya mwisho ya ujenzi wa stendi hiyo kutoka kwa Waziri Mkuu.

Alisema Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Manispaa ya Iringa liliamua kupeleka suala hilo kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda baada ya kuwepo na taarifa kutoka kwa wadau wanaoitaka halmashauri hiyo isitishe ujenzi wa stendi hiyo katika eneo hilo.

Alisema wakati suala hilo likipelekwa kwa Waziri Mkuu, tathimini ya athari za kimazingira katika eneo hilo iliyofanywa na Mtaalamu Mshauri wa Mazingira (CONSULTANT) aitwaye Arms on Environment Ltd wa Dar es Salaam inaonesha kwamba hakutakuwa na athari yoyote endapo stendi hiyo itajengwa katika eneo lililopendekezwa.

Alisema baada ya tathimini hiyo kuridhia stendi hiyo ijengwe katika eneo hilo, Juni 15, mwaka jana walipata hati ya ya ujenzi wake ambayo ni Na.EC/E15/584.

Kwa mujibu wa Mhandisi wa halmshauri hiyo, Mashaka Luhamba, mpaka kukamilika kwake stendi hiyo itagharimu zaidi ya Sh Bilioni 4 zitakazotolewa kupitia Programu ya Uendelezaji Miji inayosimamia na Ofisi ya Waziri Mkuu kwa ufadhili wa Benki ya Dunia.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment