Wednesday, 29 January 2014

MAXMALIPO, M-PESA NA TIGO PESA ZAANZA KUTUMIKA KULIPA BILI ZA MAJI IRINGA MJINI

Mkurugenzi wa IRUWASA, Marco Mfugale (kushoto) akikabidhiwa mfano wa mashine ya Max Malipo ya kulipia maji kutoka kwa Meneja Usambazaji wa Kampuni ya Maxcom Africa, Athanas Leonce wakati wa uzinduzi wa malipo ya bili za maji Iringa mjini kwa kutumia mashine hizo
WAKAZI wa Manispaa ya Iringa na Vitongoji vyake wameanza kutumia mashine za MaxMalipo kulipa bili zao za maji.

Meneja Usambazaji wa Kampuni ya Maxcom Africa, Athanas Leonce alisema mshine hizo zinaendelea kusambazwa kwa mawakala wao katika maeneo mbalimbali mjini Iringa.

Alisema kwa kupitia malipo ya bili kwa njia ya mshine hizo, IRUWASA imewatengnenezea wananchi wa manispaa ya Iringa ajira.

Leonce alisema mawakala wa mashine hizo wataweza kujiongezea kipato kupitia gawio litakalotokana na makusanyo watakayokuwa wakifanya kila mwezi.

Uzinduzi wa matumizi ya mashine hizo, ulifanywa jana katika ofisi za mamlaka hiyo katika hafla fupi iliyohudhuriwa na wanahabari, watendaji wakuu wa mamlaka hiyo na  wawakilishi wa kampuni ya Maxcom Afrika inayotoa huduma hiyo.

Mkurugenzi wa IRUWASA, Mhandis Marco Mfugale alisema kabla ya huduma hiyo wateja wao walikuwa wakilipa bili zao moja kwa moja katika ofisi yao na kwa kupitia benki ya Barclays.

“Kwasasa IRUWASA imeenda mbali zaidi ambapo mteja anaweza kulipa bili yake ya huduma ya maji kwa kupitia mashine hizo zinazotoa risiti” alisema.

Alisema wamefanikisha baada ya IRUWASA kuingia mkataba na kampuni ya Maxcom Afrika ili kumrahisishia mteja kufanya malipo hayo.

“Pamoja na mashine za Maxmalipo, wateja wa IRUWASA wanaweza kulipa bili zao kupitia M-PESA na TIGO PESA," alisema.

Alisema IRUWASA kwa kushirikiana na Maxcom Afrika iko katika hatua za mwisho za kuwawezesha wateja wanaotumia mtandao wa simu wa Airtel nao kufanya malipo yao ya maji kutimia AIRTEL MONEY.

Alisema maboresho yatawawezesha wateja wao kuokoa muda kwa kutopanga foleni katika ofisi za mamlaka na watakuwa huru kulipa wakati wowote na popote nchini.
 
Hadha hii ya kusimama kwa muda mrefu kwenye foleni, itapungua baada ya IRUWASA kuanza kutumia mshine za MaxMalipo na mitandao ya M-Pesa na Tigo Pesa kulipa bili za maji.
Kwa upande wa faida ambayo mamlaka hiyo itapata, Mfugale alisema IRUWASA itapunguza kupokea fedha nyingi ofisini na hivyo kuepuka hasara zinazoweza kusababishwa na mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na wizi.

Watendaji wa IRUWASA na Maxcom Afrika katika picha ya pamoja mara baada ya uzinduzi huo

Reactions:

1 comments: