Saturday, 1 February 2014

MWENYEKITI WA UVCCM MKOA WA IRINGA ATISHIA KUJIUZULU, BARAZA KUU LA MKOA LAMKATALIAMsowoya wakati wa harusi yake, mwaka jana

BARAZA Kuu la Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) mkoa wa Iringa lililoketi jana katika ukumbi wa Chuo cha Delima, mjini Iringa limekataa kujiuzulu kwa Mwenyekiti wake, Tumaini Msowoya.

Habari zilizotufikia hivi punde zimeeleza kwamba sintoelewana iliyojitokeza katika kikao hicho, ndiyo iliyopelekea mwenyekiti huyo achukue uamuzi wa kubwaga manyanga.

Hata hivyo jazba ya mwenyekiti huyo ‘mwanahabari’ ilitulizwa na wajumbe wa baraza hilo waliopinga uamuzi wake huo.

“Hatukubaliani na uamuzi aliotaka kuuchukua; hawezi kuucha umoja wa vijana katika kipindi hiki ambacho chama kinaelekea kwenye chaguzi ndogo tatu za udiwani mkoani hapa,” alisema mmoja wa wajumbe ambaye hakutaka jina lake lianikwe.

Februari 9, mwaka huu CCM mkoa wa Iringa itatetea viti vitatu vya udiwani vilivyokuwa wazi baada ya madiwani wake, kwa nyakati tofauti, kupoteza maisha.

Kata hizo ni Nduli iliyopo Manispaa ya Iringa, Ibumu na Ukumbi zilizopo wilayani Kilolo. Chadema ni chama pekee cha upinzani kilicosimamisha wagombea katika kata hizo.

Aidha mjumbe huyo alisema Msowoya hawezi kujiudhulu nafasi yake hiyo kwa jazba kutokana na kile alichokiita ‘majungu’ yanayopikwa na baadhi ya wajumbe wa baraza hilo.

“Kilichopelekea atishie kujiuzulu ni pamoja na majungu yanayopikwa dhidi yake na baadhi ya wajumbe wa baraza hilo; wengi wa wajumbe hawakubaliani wamekataa azma ya mwenyekiti huyo na amekubali,” alisema.

Alisema baada ya kukubaliana na maamuzi ya kikao hicho, Msowoya anaendelea na wadhifa wake huo kwahiyo ni kiongozi halali wa umoja wa vijana.

Wakati akichaguliwa, mwanahabari Tumaini Msowoya alikuwa mwakilishi wa gazeti la Mwananchi mkoani Iringa.

Alichaguliwa kwa kishindo kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) wa mkoa wa Iringa Oktoba, 2012.

Uandishi wa habari ilikuwa sifa muhimu kwake katika uchaguzi huo na kumpa nafasi ya ziada ya kukitwaa kiti hicho dhidi ya wagombea wenzake kabla ya uchaguzi huo.

Katika uchaguzi huo, jumla ya kura 302 zilipigwa ambapo
Msowoya alipata kura 188 akifuatiwa kwa mbali na Abba Ngilangwa aliyepata kura 76 huku Ramadhani Baraza akiambulia kura 36.

Alipopewa nafasi ya kuwashukuru wajumbe kwa kumpatia ushindi huo, Msowoya alisema anafahamu kazi ngumu aliyoanayo mbele yake ya kuwaangunisha vijana wa mkoa mzima wa Iringa ili kukiletea ushindi chama hicho katika Uchaguzi Mkuu wa 2015.

“Uongozi unapimwa kwa mambo mengi lakini unapokuwa katika siasa sifa kubwa ni kukisaidia chama chako kupata ushindi,” alisema huku akiomba ushirikiano kutoka kwa wadau mbalimbali wakiwemo wanahabari.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment