Friday, 5 July 2013

LOWASA APATA MAPOKEZI MAKUBWA MWANZA

WAZIRI Mkuu mstaafu, Edward Lowassa, jana alilitikisa Jiji la Mwanza baada ya kuwasili jijini hapa. Baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa jijini hapa, Lowassa alipokewa na mamia ya wananchi, viongozi wa Serikali, viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), viongozi wa madhehebu ya dini na mamia ya waendesha pikipiki. Wakati akitokea Uwanja wa Ndege kuelekea katikati ya Jiji, mamia ya wananchi walijipanga barabarani kumpokea huku wakimshangilia.

Kati ya shughuli anazotarajia kufanya leo, ni kushiriki harambee ya kuchangia fedha za kuendesha Kituo cha Redio kiitwacho IQRA FM cha jijini Mwanza.

Lengo la harambee hiyo itakayofanyika katika Hoteli ya Gold Crest ni kukifanya kituo hicho kiongeze usikivu wa matangazo yake na pia kiweze kujiendesha.

Kabla ya kuendesha harambee hiyo, Lowassa ambaye pia ni Mbunge wa Monduli (CCM), atatembelea ofisi za Umoja wa Wamachinga wa jijini Mwanza (SHIUMA) na kisha atazungumza nao.

Wakati wa harambee hiyo, Lowassa anatarajiwa kuungwa mkono na baadhi ya wabunge, makada mbalimbali wa CCM, wafanyabiashara, taasisi na kampuni mbalimbali jijini hapa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya harambee ya kituo hicho cha redio inayoongozwa na taasisi ya Kiislamu iliyo chini ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), Mkoa wa Mwanza, Shekhe Hassan Kabete, alisema maandalizi ya harambee hiyo yamekamilika kwa asilimia mia moja.

“Tuna matumaini makubwa, kwamba tutatimiza lengo la kile tunachotarajia kukifanya kwenye harambee yetu.

“Katika harambee hii, tunatarajia kukusanya zaidi ya shilingi milioni 400, ambapo tayari mfuko wetu umeshakusanya kiasi cha shilingi milioni 190.

“Kwa hiyo, kwa kuwa tunaamini Lowassa ni jembe la Watanzania, lengo letu litafikiwa na pengine kuvuka kwa sababu pia tunamtegemea Mungu katika mambo yetu,” alisema Shekhe Kabete.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment