Sunday, 30 December 2012

MINJINGU MAZAO YAPIGIWA DEBE NA PROF MSOLLA

Prof Peter Msolla


MBUNGE wa Jimbo la Kilolo, Profesa Peter Msolla amefanya ziara katika vijiji vya Iswaga, Mlafu na Itungu jimboni humo akihamasisha matumizi ya mbolea ya Minjingu Mazao.

“Mbolea hii ina virutubisho zaidi ya vile vilivyoko kwenye mbolea aina ya DAP mliyoizoea. Minjingu Mazao ni tofauti kabisa na mbolea ya Minjingu iliyoletwa misimu iliyopita,” alisema.

Alisema tafiti zilizofanywa kabla haijaingizwa sokoni, zinaonesha mbolea ya Minjingu Mazao ina ubora kama wa DAP.

“Ili kuleta mapinduzi ya kijani kupitia kilimo kwanza, serikali inataka wakulima wake wapate pembejeo bora na kwa bei watakazoweza kuzimudu,” alisema.

Alisema mbolea ya Minjingu Mazao inauzwa kwa Sh 32,000 tofauti na DAP inayouzwa kati ya Sh 75,000 na Sh 80,000 kwa ujazo ule ule.

“Gharama kwa wakulima waliopo katika mfumo wa ruzuku ya pembejeo ni ndogo zaidi kwani wao wanatoa Shilingi 24,000 kwa mifuko miwili na serikali inawachangia Shilingi elfu arobaini,” alisema.

Ili kufikia mahitaji ya msoko mbalimbali, Profesa Msolla alisema serikali ina mpango wa kuona kampuni za uzalishaji mbolea zinaingiza bidhaa hizo zikiwa katika ujazo tofauti.

“Wapo wakulima wanataka kilo kumi, wengine ishirini wengine hamsini, kwahiyo kuna haja ya kuzingatia mahitaji ya wakulima kulingana na uwezo wao,” alisema.

Akiwa katika kijiji cha Iswaga, Profesa Msolla aliambiwa na wananchi wa kijiji hicho kwamba wanaogopa kutumia mbolea ya Minjiungu Mazao kwasababu haijazoeleka.

“Imeletwa lakini hatujatumia kwasababu tulikuwa hatuna taharifa kama Minjingu Mazao ina virutubisho kama vya DAP tuliyoizea,” alisema Muhabu Lwanzali aliyesoma risala ya kijiji hicho.

Ruben Mwambelo alimshukuru mbunge kwa elimu hiyo aliyosema ilipaswa kutolewa na maafisa ugani kabla msimu wa kilimo haujaanza.

Hata hivyo William Masika alisema, wakati taarifa ya Mbunge inaonesha kwamba wanaopata pembejeo za ruzuku wanatakiwa kuchangia Sh 24,000 kwa mifuko miwili, katika kijiji hicho wakulima hao wanatakiwa kuchangia Sh 35,000.

Mmoja wa Maafisa Kilimo na Ushirika wa Halmashauri hiyo, Edward Mbembe alisema katika mikutano hiyo kwamba ongezeko la bei hiyo linatokana na gharama za usafirishaji.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment