Friday, 27 May 2016

CHUMI AKATAA KUMSAMEHE WILLIAM MUNGAI


MBUNGE wa Jimbo la Mafinga Mjini, Cosato Chumi amekataa kumsamehe aliyekuwa mgombea wa jimbo hilo kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), William Mungai anayedaiwa kuwatumia baadhi ya wanasiasa kuomba asamehewe kulipa gharama za kesi ya uchaguzi.

Mungai ambaye ni mmoja wa watoto wa Joseph Mungai ambaye kwa zaidi ya miaka 20 alikuwa mbunge wa jimbo la Mufindi Kaskazini na waziri katika serikali ya awamu ya kwanza hadi ya nne alifungua kesi kupinga matokeo yaliyompa ushindi Chumi baada ya kushindwa uchaguzi huo wa 2015.

Kesi hiyo namba 8 ya mwaka 2015 ilitupiliwa mbali na Mahakama Kuu Kanda ya Iringa Mei 3, mwaka huu baada ya kukosekana kwa ushahidi wa kutosha kutengua matokeo hayo.

Akizungumza na wapiga kura wa jimbo lake kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika hivikaribuni katika uwanja wa Mashuja mjini Mafinga, Chumi alisema; “mimi ni mtoto wa masikini siwezi kuwasaliti wananchi wanyonge, mmeniamini na kunichagua kuwa mbunge wenu, niwaahidi sitawaangusha.”

“Niwashukuru tumekuwa pamoja katika kipindi hicho kigumu cha kesi baada ya wenzetu kwenda mahakamani kupinga matokeo ya ubunge ulionipa ushindi, lakini Mungu alikuwa nasi na tukashinda kesi hiyo baada ya ukweli kubainika,” alisema.

Alisema wakati kesi hiyo ikiendelea, wananchi wa Mafinga waliwekwa roho juu na baadhi ya wanasiasa waliokuwa wakiombea ashindwe kesi hiyo ili uchaguzi urudiwe.

Alisema baada ya kushindwa kesi hiyo, wameanza kutuma watu wakisema wao wote ni vijana kwahiyo wasameheane jambo ambalo hayuko tayari kulifanya.

“Leo mawakili wangu wameanza kuandaa mchanganuo wa gharama za kesi. Ni lazima watulipe maana katika hili tumepoteza muda na rasilimali nyingi. Kuna watu walitaka kutusaidia lakini walisitisha misaada yao baada ya kesi hiyo kufunguliwa,” alisema.


“Kwa kweli mimi ni mkristo kweli kweli lakini katika hili hata Mungu hawezi kulibariki. Kwahiyo niseme siwezi kusamehe kwasababu kesi hiyo imeturudisha nyuma kwenye mambo mengi sana,” alisema.

IRINGA YAANZA MSAKO WA WALIMU WANAOFANYA NGONO NA WANAFUNZI WAO WA KIKE


TAARIFA za walimu wanaofanya mapenzi na wanafunzi wao wa kike katika shule mbalimbali za msingi na sekondari wilayani Iringa zinazidi kumiminika katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Iringa inayoendelea kuzifanyia kazi.

Akizungumza na wanahabari juzi, Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela alisema; “tunapokea taarifa za kusikitisha zinazowahusisha baadhi ya walimu katika shule zetu kufanya mapenzi na watoto wetu, hili ni jambo la kusikitisha.”

Kasesela alisema baadhi ya wanafunzi hao wanafanya mapenzi na walimu wao kwa kulazimishwa na kubakwa huku wakipewa vitisho mbalimbali vikiwemo vya kufelishwa mitihani yao.

Alisema Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya hiyo kwa kushirikiana kwa jirani na jeshi la Polisi imeanza kuzifanyia kazi taarifa hizo.

Alisema walimu watakaobainika kujihusisha na vitendo hivyo watachukuliwa hatua za kinidhamu na kisheria kwa mujibu wa sheria za utumishi na nchi.

“Tayari tumeanza kazi ya uchunguzi wa taarifa hizo katika shule tatu kati yake mbili za mjini na mmoja ipo Iringa Vijijini,” alisema bila kuzitaja shule hizo ili kutovuruga ushahidi.

Alitoa wito kwa wanafunzi wanaolazimishwa na walimu hao kufanyiwa vitendo hivyo kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa za siri katika ofisi yake au Polisi.

“Huu ni udhalilishaji mkubwa, hatuwezi kuwavumilia walimu wenye tabia kama hizo na tutajitahidi kupata taarifa zao na kuwachukulia hatua ili kutoa fundisho kwa wengine,” alisema.


Aliwataka wazazi na walezi wa wanafunzi kuzingatia jukumu lao la malezi bora kwa watoto wao ili kuwaepusha na vishawishi vinavyowza kuwaingiza katika matukio yanayoweza kuwaharibu kitaaluma na kimaisha.

DADA WA BILIONEA AUAWA KWA KUCHINJWA


Mtumishi wa Wizara ya Fedha, Aneth Msuya (30) ambaye ni mdogo wa Bilionea Erasto Msuya aliyeuawa kwa kupigwa risasi 22 KIA, ameuawa kwa kuchinjwa nyumbani kwake eneo la Kigamboni jijini Dar Es Salaam.

Mmoja wa ndugu wa familia hiyo, Shujaa Khamis, jana alithibitisha kuuawa kwa Aneth, lakini alikataa kuingia kwa undani.

“Ni kweli wamemchinja usiku wa kuamkia leo (jana) na hapa nipo kwenye msiba hapa nyumbani (Mererani) kwa baba. Tumeambiwa wamechukua Tv tu,” alisema.

Hata hivyo, Khamis alikataa kueleza lolote kama wana mashaka na mauaji hayo zaidi ya kuliomba Jeshi la Polisi nchini, kuchunguza kiini cha mauaji hayo na kuwasaka waliohusika.

Habari nyingine kutoka Wizara ya Fedha, ziliwakariri baadhi ya watumishi wakisema wamepata taarifa za msiba huo, lakini hawajapewa taarifa rasmi.

“Tuna taarifa tunazisikia sikia kuwa ameauawa, lakini jana (juzi) tulikuwa naye kazini ila leo (jana) ndiyo tunasikia amechinjwa na watu wasiojulikana.

Imetusikitisha sana,” alisema mmoja wa watumishi hao ambaye hakutaja jina kwa kuwa si msemaji.

Kamanda wa mkoa wa Kipolisi wa Temeke, Andrew Satta alipofutwa jana kuthibitisha taarifa za mauaji hayo alisema yuko kwenye kikao.


WAZEE TTCL WATAKIWA KUWAPISHA VIJANA KUMUDU USHINDANI


Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa amesema wakati umefika kwa wazee wanaofanya kazi katika Kampuni ya simu ya TTCL kuwaachia Vijana kwa kuwa sekta ya Mawasiliano hivi sasa ina ushindani mkubwa.

Akizindua nembo mpya ya kampuni hiyo na mtandao unaotumia teknolojia ya 4G LTE jana, Prof Mbarawa alisema wazee wamekua watu wa kuzungumza zaidi ofisini kuliko kufanya kazi na kubuni mbinu mpya zenye kuhimili ushindani.

“Uzinduzi huu hautakuwa na maana ikiwa wafanyakazi wa kampuni hii hawatabadilika na kutoa huduma zinazovutia wateja,” alisema.

Pia Prof. Mbarawa aliishauri menejimenti kutoajiri watumishi kwa kujuana, bali watoe fursa kwa Vijana wenye uwezo wa kuhimili ushindani unaotokana na mabadiliko ya teknolojia ya Mawasiliano.


Mwakilishi wa mwenyekiti wa bodi ya kampuni hiyo, Edwina Lupembe alisema TTCL wakati wowote kuanzia sasa itaanzisha huduma ya usafirishaji wa fedha kama zilivyo kampuni nyingine za simu za mkononi.

Thursday, 26 May 2016

WILAYA YA IRINGA YAJIPANGA KUDHIBITI MAUAJI, UBAKAJI NA BODABODA


VITENDO vya ubakaji na mauji wilayani Iringa, vimeelezwa na mkuu wa wilaya hiyo, Richard Kasesela kuanza kuota mizizi inayohatarisha sifa ya amani na furaha iliyopo katika eneo hilo.

Pamoja na vitendo vya ubakaji na mauaji, Kasesela ameelezea changamoto za usafiri wa bodaboda katika wilaya yake kwamba umeongeza ajali, uvunjishu wa sheria za barabarani, ujambazi na mauaji.

Akizungumza na wanahabari jana, amelitaka jeshi la Polisi kuzidisha juhudi kwa kuhakikisha watuhumiwa wa matukio hayo wanakamatwa bila kujali wingi wao na kufikishwa katika vyombo vya dola.

“Tunajua mahabusu zetu ni ndogo, tutaomba kutumia ukumbi wa jumba la maendeleo la mjini Iringa kuwahifadhi matuhumiwa watakaokuwa wanakamatwa kutokana na matukio mbalimbali ya kihalifu tukilenga kuusafisha mji na wilaya yetu” alisema.

Akizungumzia matukio ya mauaji mkuu wa wilaya huyo ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Iringa alisema kwa taarifa za siku mbili zilizopita raia wawili wameuawa baada ya wananchi kujichukulia sheria mkononi, na wengine watatu wamefariki katika matukio ya ujambazi, wivu wa kimapenzi na ubakaji.

Akizungumzia tukio la ubakaji, Kasesela alisema wananchi wa eneo la Mtwivila mjini Iringa, walimshambulia mwananchi mmoja aliyefahamika kwa jina la Emanuel (30) kwa tuhuma za kubaka mtoto wa miaka 10 na kumpiga mawe hadi kufariki.

Kuhusu ubakaji alisema katika kipindi kifupi kilichopita kumeibuka wimbi la ubakaji wa watoto chini ya miaka 14 linalokabiliwa na tatizo la ukusanyaji wa ushahidi na uendeshaji wa kesi zake.

“Makundi manne yaani jeshi la Polisi, ofisi ya mwanasheria mkuu, mahakama na madaktari wanatupiana lawama katika kutekeleza wajibu wao wa kuwashughulikia wabakaji na kusababisha wahanga wa ubakaji waendelee kuteseka,” alisema.

Ili kusaidiana na kukabiliana na vitendo hivyo aliwataka wazazi kusaidia jukumu la kuwalinda watoto na kuwatunza

Akizungumzia changamoto ya bodaboda mjini hapa alisema uanzishwaji wake ulikuwa wa nia njema ukilenga kupunguza changamoto ya ajira nchini.

“Mbali na ajali zinazosababishwa na bodaboda kutokana na uvunjishu wa sheria za barabarani, zimekuwa  zikutumika katika matukio ya wizi na uporaji na kusababisha baadhi yao kuuawa,” alisema.


Ili kukomesha matukio ya kiharifu yanayosababishwa na bodaboda, mbinu mbadala ya kuwabadilisha madereva wake fikra ili watii sheria na kuwa na muda maalumu wa kufanya biashara hiyo, inatafutwa na watatakiwa kutambuliwa katika vituo vyao kwa kuwa na daftari lenye picha zao.

Wednesday, 25 May 2016

Shule zote zisizosajiliwa kufungwa

Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk Leonard Akwilapo
SHULE zote ambazo hazijasajiliwa zimepewa miezi miwili ziwe zimesajiliwa, kabla ya serikali kuzifunga baada ya muda huo kuisha.
Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk Leonard Akwilapo alisema hayo jana.

Kwamba ifikapo Julai 30 mwaka huu, mmiliki wa shule itakayobainika kutosajiliwa, ikiwemo zitakazokosa vigezo vya kusajiliwa, atapaswa kuhamisha wanafunzi waliopo kwa gharama zake.
Alisisitiza wahusika wasajili shule hizo kabla ya tarehe hiyo. Alisema kuwa agizo hilo ni kutekeleza Sheria ya Elimu Sura ya 353, inayoelekeza shule zote kusajiliwa kabla ya kusajili wanafunzi.
Akwilapo alisema kwa kutofuata utaratibu huo wa kusajili shule, wanafunzi wanaotoka katika shule au vituo hivyo hufanya mitihani ya taifa, ikiwemo mtihani wa maarifa (QT) na mitihani mingine ya taifa (Kidato cha Nne na Sita) kama watahiniwa wa kujitegemea.
Alisema pia baadhi ya wanafunzi hao huingizwa kwa utaratibu usio rasmi, kufanya mitihani ya Darasa la Nne na Darasa la Saba katika shule zilizosajiliwa bila kuzingatia mazingira ya mahali waliposomea, hali inayochangia kwa kiasi kikubwa kushindwa katika mitihani hiyo.
“Wamiliki wote wa shule ambazo hazijasajiliwa wanatakiwa kuwasilisha maombi yao katika Ofisi za Uthibiti Ubora wa shule Kanda, Wilaya au Idara ya Ithibati ya shule (Usajili) Makao Makuu ya wizara kabla au ifikapo Julai 30 mwaka huu,” alisema.
Alipoulizwa ni shule ngapi ambazo zinajiendesha bila kusajiliwa, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ithabati ya Shule, Khadija Mcheka alisema: “Hapa nilipo sitaweza kukupa takwimu sahihi, lakini kwa mkoa wa Dar es Salaam tumeshafungia shule za awali na msingi zipatazo 23.” “Tatizo kubwa lipo kwenye shule za awali na msingi ndio nyingi ambazo zinatoa huduma ya elimu bila kusajiliwa, kwa shule za sekondari ni kidogo,” alisema.

Hali ya sukari sasa ahueni


HALI ya upatikanaji sukari nchini, imeanza kuwa kwenye mwelekeo mzuri, baada ya tani zaidi ya 10,000 kuingizwa kutoka nje. Nyingine 31,000 zinasubiriwa kuwasili huku viwanda vya bidhaa hiyo pia vikianza uzalishaji wiki hii.
Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage alitoa taarifa hiyo jana bungeni wakati mjadala wa bajeti ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ukihitimishwa.
Akielezea sukari inayoingia kutoka nje, Mwijage aliwataka wafanyabiashara wote wanaojishughulisha na bidhaa hiyo, kujitambulisha kwa wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya ili wanayopewa Dar es Salaam, waifikishe kwa viongozi hao waione.
Kuhusu viwanda ambavyo awali vilitarajiwa kuanza uzalishaji Julai mwaka huu, Mwijage alisema, “Adha ya sukari iliyokuwepo, sasa inakwenda kuisha. Kuna sukari ya kutosha…kwani leo kiwanda cha Kagera Sugar kimeanza kuzalisha tani 250.”
Waziri Mwijage alisema pia Kiwanda cha Kilombero (K One), kimeanza kuzalisha na kitazalisha tani 600 kwa siku. Wakati matumizi ya nchi ni tani 1,200 za sukari kwa siku, Mwijage alisema tofauti iliyobaki ndiyo imeagizwa kutoka nje.
Aliwataka wabunge kutambua kuwa uamuzi uliochukuliwa na serikali, ulijenga imani na kuleta wawekezaji. Alisema hivi sasa, Kiwanda cha Sukari Kagera kinapanua eneo la Kitegule na kuzalisha tani nyingine 60,000 na pia kukiwa na mwekezaji kutoka Oman, ambaye ataongeza uzalishaji katika kiwanda hicho na kufikia tani 300,000.
Alisema adha ya sukari ambayo nchi inapitia sasa ni kwa ajili ya kudhibiti uingizaji sukari na kisha kuleta wawekezaji kwenye uzalishaji wa sukari. Mwijage alisema hali ya sukari ni ya kutosha na sasa wamechukua hatua ya kujenga kiwanda cha Kigoma Sugar katika eneo la hekta 47,000.

Majaliwa: Tanzania kuiuzia umeme Zambia

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Tanzania ina mpango wa kujenga njia ya umeme kutoka Mbeya hadi Zambia kupitia Tunduma ili kupunguza tatizo la umeme linaloikabili nchi hiyo.
“Serikali ya Tanzania inajenga njia ya umeme ya msongo wa KV 400 kutoka Iringa - Dodoma – Singida – Shinyanga ambayo ni sehemu ya mradi mkubwa wa umeme unaolenga kuunganisha Zambia, Tanzania na Kenya,” alisema.
Alisema upembuzi yakinifu kwa ajili ya KV400 kutoka Iringa hadi Mbeya, umekamilika tangu mwaka 2012, na hivi sasa Serikali inatafuta fedha kwa ajili ya kuunganisha kipande cha kutoka Mbeya na gridi ya Taifa ya Zambia.
Waziri Mkuu ambaye anahudhuria katika Mkutano wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwenye Kituo cha Mikutano cha Mulungushi kilichopo Lusaka, Zambia kwa niaba ya Rais John Magufuli, alitoa ufafanuzi huo jana mchana wakati akichangia hoja kwenye mjadala wa wakuu wa nchi na Serikali uliohusu Nishati na Mabadiliko ya Tabianchi kwenye ukumbi wa mikutano cha kimataifa wa Mulungushi.
Alisema ili kukabiliana na changamoto ya nishati barani Afrika, nchi za bara hili zinahitaji kuwa na fedha ama mitaji, teknolojia ya kisasa na wataalamu wenye ujuzi wa kutosha, jambo ambalo amesema ni gumu kulikamilisha kila nchi peke yake.
Alisema ili kukaribisha wawekezaji kwenye sekta ya umeme, Tanzania inafanyia marekebisho sheria zake ili kuruhusu uwekezaji kwenye sekta hiyo.
Akizungumzia kuhusu hali ya nishati nchini Tanzania, Waziri Mkuu alisema Tanzania imebarikiwa kuwa na gesi asilia yenye ujazo wa futi trilioni 57.25 (tcf), makaa ya mawe yenye ujazo wa tani bilioni 1.9 (asilimia 25 imevumbuliwa), umeme wa nguvu ya maji wa gigawati 4.7 ambazo ni asilimia 12 tu ndiyo inatumika.